IQNA

Misahafu 1,500 Yagawanywa kwa Wanafunzi wa Madrasa nchini Chad

19:44 - May 25, 2026
Habari ID: 3482282
IQNA – Wanafunzi wa madrasa nchini Chad wamezawadiwa Misahafu au nakala 1,500 za Qur’ani Tukufu na taasisi ya kutoa misaada ya nchini Uturuki inayojulikana kama Orphan Foundation (Yetimler Vakfı).

Taasisi hiyo imefanikiwa kupanua kampeni yake endelevu ya kielimu na kibinadamu nchini Chad, kwa kugawa nakala hizo 1,500 za Qur’ani Tukufu kwa wanafunzi katika madrasa saba tofauti zilizoko vijijini, katika vitongoji vya mji mkuu wa N’Djamena.

Mpango huu unawalenga hasa watoto wa kiume na wa kike wanaopitia mafunzo magumu ya kuhifadhi Qur’ani (Hifdhu) katika mazingira yenye changamoto kubwa za kimaisha. Kwa kufadhiliwa kikamilifu na michango ya wafadhili na wenye kutoa sadaka kutoka kote duniani, ugawaji huu unalenga kupunguza upungufu mkubwa wa rasilimali za kielimu katika wilaya za vijijini mwa nchi hiyo.

Maafisa wa taasisi hiyo wamesisitiza kuwa uwepo wao nchini Chad ni sehemu ya mkakati wa kudumu wa mwaka mzima, na si msaada wa msimu wa Sikukuu pekee. Katika tathmini za nyanjani zilizofanywa hivi karibuni, timu za wajitoleaji zilibaini changamoto kubwa za kimfumo na kielimu ndani ya mfumo wa madrasa za eneo hilo, hali iliyopelekea ahadi ya kuanza utoaji wa misaada zaidi kwa hatua.

“Msaada wa kielimu ni wenye umuhimu wa kipekee kwa mustakabali wa watoto hawa,” alisema Mehmet Ali Aysu, Mwakilishi wa Orphan Foundation anayeongoza shughuli hizo nchini humo. “Ugawaji wetu wa Qur’ani Tukufu na msaada wetu wa moja kwa moja kwa madrasa hizi utaendelea bila kukatizwa.”

Bwana Aysu alisisitiza kuwa lengo kuu la taasisi hiyo linabaki kuwa kuhakikisha fursa za elimu zinapatikana kwa watoto yatima, wasio na baba, na wale wanaotoka katika familia duni kiuchumi ambao mara nyingi huachwa nyuma na mifumo ya kawaida ya elimu.

Akizungumzia mipango ya baadaye, Orphan Foundation imetangaza azma ya kuongeza wigo wa operesheni zao nchini Chad, kukiwa na miradi mipya kadhaa ya kielimu na kijamii iliyopangwa kuanza katika miezi ijayo, kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu.

3497592

Kishikizo: CHAD qurani tukufu
captcha