IQNA

Imam Khamenei

Taifa la Iran halitasalimu amri mbele ya mabavu ya Marekani

13:22 - February 18, 2014
Habari ID: 1376766
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei Jumatatu alihutubia maelfu ya wananchi wa miji mbalimbali ya mkoa wa Azarbayjan Mashariki waliokwenda kuonana naye akilishukuru taifa la Iran kwa kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (Februari 11) ya kuadhimisha miaka 35 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.

Kwa mujibu wa  Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, amesema maandamano hayo yalikuwa na ujumbe mbili ambazo ni kusimama kidete na umoja. Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran lilihudhuria kwa wingi katika maandamano ya tarehe 22 Bahman katika kujibu ufidhuli, sera za kupenda kujitanua, utovu wa adabu na kiburi cha viongozi wa Marekani, na kutangaza kuwa kamwe halitasalimu amri mbele ya sera za mabavu za Marekani.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 36 wa harakati ya kihistoria ya wananchi wa Tabriz hapo tarehe 29 Bahman mwaka 1356 Hijria Shamsia (…), Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu  alianza hotuba yake kwa kuwashukuru wananchi kwa kuhudhuria kwa wingi katika maandamano ya Februari 11. Amesema, ulimi hauwezi kulishukuru taifa kubwa la Iran lakini kwanza kabisa tunamshuruku Mwenyezi Mungu anayebadili hali na nyoyo za watu, na pili tunawashukuru wananchi wa Iran kote nchini kwa kuonesha sura safi, yenye kung'ara na hai ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa walimwengu
Baada ya hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia harakati ya tarehe 29 Bahman ya wananchi wa Tabriz na kusema kuwa, tukio hilo lilikuwa na ibra na mafunzo mengi. Amesisitiza kuwa somo la kwanza la harakati hiyo ni kuonesha sifa za kipekee za watu wa Tabriz na Azarbaijan.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, imani kubwa ya kidini, ghera ya dini, ushujaa, kutambua alama za nyakati, kuchukua hatua wakati mwafaka, ujasiri na ubunifu katika njia ya malengo ni miongoni mwa sifa za watu wa Tabriz na Azarbaijan zilizoonekana tarehe 29 Bahman.
Somo la pili lililotajwa na Ayatullah Khamenei la harakati ya tarehe 29 Bahman ni kuonesha msikamano na mfungamano wa maeneo na kaumu mbalimbali hapa nchini. Amesema kuwa, kaumu mbalimbali za Iran zimekuwa chini ya bendera ya Uislamu na jina zuri la Iran kupitia utawala wa Kiislamu na zote hizo zina mfungamano na umoja, suala ambalo limekuwa likiwatia kiwewe watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran na wanaotaka kaumu za Kiirani zikabiliane.
Amewataka wananchi na viongozi wote hapa nchini kuwa macho na kusisitiza kuwa, ujumbe wa umoja na mshikamano wa harakati ya tarehe 29 Bahman haupaswi kusahaulika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja "muujiza wa irada na azama ya taifa" kuwa ni somo la tatu la harakati ya tarehe 20 Bahman na kusisitiza kuwa, harakati hiyo imeonesha kuwa, hakuna kizuizi wala dola lolote kubwa linaloweza kusimama mbele ya idara na azma kubwa ya taifa.
Akichambua sababu za mahudhurio makubwa ya wananchi katika maandamano ya Februari 11 mwaka huu na ujumbe wa mahudhurio hayo, Ayatullah Khamenei ameashiria mahesabu na ripoti za kuaminika za wataalamu kuhusu kiwango cha mahudhurio hayo katika miaka mbalimbali na kusema kuwa, kwa mujibu wa ripoti za kuaminika za wataalamu, idadi ya watu walioshiriki katika maandamano ya mwaka huu kote nchini ni kubwa zaidi kuliko mwaka uliopita na hii ni ishara kuwa, sherehe za kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni tukio lisilo na kifani, kama yalivyo mapinduzi yenyewe.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kufanyika sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali nchini tena katika mwaka wa 35 wa mapinduzi hayo, tofauti na sherehe kavu na rasmi zinazofanyika katika nchi nyingine, ni tukio la kustaajabisha. Ameongeza kuwa, kinyume na propaganda chafu na uchambuzi usio sahihi wa vyombo vya habari vya kigeni, vituo vyao vya fikra vinapokea ujumbe wa mahudhurio makubwa, ari, imani na kaulimbiu zilizotolewa na wananchi wa Iran katika maandamano hayo.
Ayatullah Khamenei amesema kaulimbiu za wananchi katika maandamano ya tarehe 22 Bahman ilikuwa na ujumbe mbili kuu ambazo ni kusimama kidete na umoja. Amebainisha ujumbe wa kusimam kidete na kushikamana na thamani na malengo ya Mapinduzi na kusema kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu yana thamani za ndio na hapana. Thamani za ndio ni kutekeleza sheria za Uislamu, kutekeleza uadilifu wa kijamii, mahudhurio ya wananchi katika nyanja na matukio mbalimbali, kuwa na uchumi unaojitegemea, kuwa na utamaduni usiokuwa tegemezi na asili wa Kiirani- Kiislamu, kuwalinda na kuwatetea wanaodhulimiwa, kupambana na madhalimu, ustawi wa nchi, maendeleo ya kisayansi na kuwa mbele katika maadili na masuala ya kiroho.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kutosalimu amri mbele ya sera za mabavu za mfumo wa kibeberu unaoongozwa na Marekani ni miongoni mwa thamani za hapana za Mapinduzi ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa tarehe 22 Bahman (Februari 11 mwaka huu) taifa la Iran lilitangaza kuwa halitasalimu amri mbele ya sera za kibeberu na kimabavu za Marekani.
Amekosoa juhudi zinazofanywa na baadhi ya watu za kutaka kuonesha sura isiyokuwa halisi ya Marekani kwa wananchi na kusema: "Baadhi ya watu wanafanya jitihada za kupamba sura ya Marekani na kusafisha maovu na ukatili wa nchi hiyo na kuiarifisha serikali ya Marekani kuwa inawapenda wananchi wa Iran na inahudumia malengo ya kibinadamu, lakini juhudi hizo hazitafaulu."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia mbaya ya serikali ya Marekani katika kipindi cha kwa uchache miaka 80 ya hivi karibuni na kusema kuwa: Miongoni mwa vitendo vya faili jeusi la Marekani ni kuanzisha vita vya umwagaji damu na kuua watu wasio na hatia, kuwaunga mkono madikteta madhalimu katika maeneo mbalimbali duniani, kuunga mkono ugaidi wa kimataifa, kuunga mkono ugaidi wa kiserikali ambao dhihirisho lake kuu ni utawala bandia, ghasibu na unaotenda jinai wa Israel, kushambulia Iraq na kuua kwa uchache maelfu ya makumi ya watu wasio na hatia, kuishambulia Afghanistan na kuanzisha mashirika ya kuua watu kama lile la Black Water na makundi ya takfiri yenye misimamo mikali na kuyaunga mkono.

1376180

captcha