IQNA

Ubaguzi dhidi ya Waislamu huko Ubelgiji

20:30 - February 25, 2014
Habari ID: 1380048
Kamati ya Kufuta Ubaguzi ya Umoja wa Mataifa imeikosoa serikali ya Brussels kutokana na mwenendo wake wa kinyonga katika kuanzisha taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, Kamati hiyo sambamba na kukosoa utendaji wa kibaguzi na wa utumiaji mabavu wa polisi ya Ubelgiji, imelalamikia maandamano ya kibaguzi na yaliyo dhidi ya Uislamu nchini Ubelgiji na uzembe katika kushughulikiwa mashtaka. Imekuja katika ripoti ya Kamati ya Kufuta Ubaguzi kwamba, wahajiri wamekuwa wakifanyiwa vitendo vibaya na kutimuliwa nchini humo. Wimbi jipya la kueneza chuki dhidi ya Uislamu liliibuka nchini Ubelgiji baada ya kuchaguliwa Waislamu wawili katika uchaguzi wa Mabaraza ya Miji mjini Brussels. Utafiti uliofanywa kuhusiana na vitendo vya kueneza chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya unaonesha kuongezeka vitendo hivyo hususan nchini Ubelgiji. Taasisi ya Haki za Binadamu ya Waislamu nchini Ubelgiji hivi karibuni ilitoa ripoti ya utafiti wake kuhusiana na vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu. Ripoti hiyo inaonesha kuwa, takriban Waislamu laki sita nchini Ubelgiji wanakabiliwa na vitendo mbalimbali vya kibaguzi hususan katika maeneo ya kazi, katika sekta ya elimu na huduma za jamii. Ripoti hiyo aidha inaonesha kwamba, njama dhidi ya Uislamu na Waislamu ziliongezeka mno katika mwaka uliopita wa 2013. Zaidi ya mashtaka 700 ya vitendo vya kibaguzi na kueneza chuki dhidi ya Uislamu yaliwasilishwa na kuandikishwa katika vituo vya polisi ambapo asilimia 27 kati ya vitendo hivyo vilihusiana na sekta ya elimu, asilimia 24 katika maeneo ya kazi na asilimia 15 ilihusiana na ubaguzi katika vyombo vya habari na magazeti. Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International mara kadhaa limekosoa na kulalamikia vitendo vya kibaguzi dhidi ya Waislamu barani Ulaya. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, licha ya kuweko wimbi kubwa la hujuma na propaganda za vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya matukufu ya Kiislamu, lakini Uislamu ndio dini yenye wafuasi wengi zaidi barani Ulaya baada ya Ukristo na idadi ya watu wanaosilimu na kuingia katika dini hii tukufu imekuwa ikiongezeka kila siku katika nchi za Magharibi.

1379778

captcha