IQNA

Siasa

Assadollah Assadi, mwanadiplomasia Muirani aliyekamatwa Ubelgiji arejea nchini

12:46 - May 27, 2023
Habari ID: 3477051
TEHRAN (IQNA)- Assadollah Assadi, mwanadiplomasia wa Iran ambaye alikuwa akishikiliwa kinyuma cha sheria gerezani nchini Ubelgiji amerejea Tehran siku ya Ijumaa.

Mnamo Julai 2018, mwanadiplomasia huyo wa Iran alikamatwa kinyume cha sheria katika jimbo la Bavaria, Ujerumani, alipokuwa akirejea katika makazi yake mjini Vienna, Austria ambapo licha ya kuwa na kinga ya kidiplomasia alikabiliwa na tuhuma za kupanga shambulizi dhidi ya mkutano wa kundi la kigaidi la MKO  nchini Ujerumani. Alihamishiwa Ubelgiji mnamo Oktoba 2018 baada ya siku mia moja na moja ya kukamatwa kwake kwa amri isiyo halali ya mahakama ya Karlsruhe ya Ujerumani.

Baada ya uhamisho huo, mahakama ya Antwerp nchini Ubelgiji, kinyume na kinga ya kidiplomasia ya Assadi chini ya Mkataba wa Vienna wa 1961, ilimhukumu kifungo cha miaka ishirini jela, hukumu ambayo ilikuwa kinyume cha sheria.

Baada ya takriban miaka 5, Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman ilitangaza jana Ijumaa kwamba Muscut imefanikiwa kupatanisha Ubelgiji na Iran kutatua suala la raia wa nchi mbili waliofungwa. 

Iran ilimwachilia huru Mbelgiji, Olivier Vandecasteele, ambaye alikamatwa katika ziara yake nchini Iran mnamo Februari 2022 na kuhukumiwa miaka 40 jela na kuchapwa viboko 74 kwa tuhuma kadhaa zikiwemo za ujasusi. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Wanafunzi wa Iran ; Ijumaa hii jioni, ndege iliyombeba mwanadiplomasia huyo wa Iran iliwasili katika uwanja wa ndege wa Imam Khomeini mjini Tehran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, akitangaza kuachiliwa huru mwanadiplomasia huyo wa Iran, alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema: "Namshukuru Usultani wa Oman kwa juhudi zake chanya katika mwelekeo huu."

4143666

captcha