IQNA

'Karibu Waislamu wote wamefukuzwa Bangui, CAR'

6:50 - March 09, 2014
Habari ID: 1384500
Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesema karibu Waislamu wote waliokuwa wakiishi mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, wamelazimika kuondoka mjini humo kutokana na jinai za magaidi wa Kiksristo.

Kwa mujibu  wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya misaada ya kibinaadamu Bi. Valerie Amos amesema idadi ya Waislamu ilikuwa kati ya 130,000 hadi 145,000 na kuteremka hadi 10,000 mwezi Desemaba mwaka jana. Ameongeza kuwa idadi hiyo sasa imepungua chini ya Waislamu 900 pekee. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka  vikosi zaidi vya kulinda amani vitumwe  katika nchi hiyo ili kutuliza hali ya mambo. Siku ya Alkhamisi pia Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) Antonio Guterres alilaani mauaji ya kuangamiza kizazi yanayofanyika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo. Guterres alisema jana kuwa Waislamu wengi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamelazimika kuikimbia nchi yao kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo. Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanasema kuna njama za makusudi za kuwaangamiza kwa umati Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Maelfu ya Waislamu wameuawa, Misikiti imebomolewa na nyumba na maduka ya Waislamu kuporwa na magaidi wa kundi la kikristo la Anti Balaka. Kuna askari karibu 2,000 wa Ufaransa na maelfu ya askari wengine wa kulinda amani kutoka nchi za Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini wameshindwa kuzuia mauaji ya Waislamu yanayofanywa na magaidi wa kundi la anti-Balaka.

1384353

captcha