IQNA

Sheikhe Mkuu wa Al Azhar: Matakfiri wanauharibia jina Uislamu

12:10 - May 15, 2014
Habari ID: 1407014
Magaidi wa Kitakfiri au Kiwahabbi ambao wanajifanya kuwa Waislamu sasa wanatekeleza jinai katika maeneo mbali mbali ya dunia kwa lengo la kuuharibia jina Uislamu. Hayo yamedokezwa na Shekhe Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar nchini Misri, Ahmad Tayyib.

Mwanazuoni huyo mwandamizi wa ulimwengu wa Kiislamu amenukuliwa na tovuti ya albawabhnews akisema kuwa wale walioingia katika mtego wa matakfiri wanatumiwa kukausha mizizi ya utamaduni wa Uislamu sahihi. Sheikh Ahmad Tayyib ameongeza kuwa watu hao waliopotea wanatoa fatuwa zisizo sahihi na zilizo mbali kabisa na misingi ya Uislamu. Katika mahojiano na Televisheni ya Al Hayati, Sheikh Ahmad Tayyib amesikitika kuwa hivi sasa kuna mapigano baina ya madhehebu za Kiislamu na kuongeza kuwa Chuo Kikuu cha Al Azhar kinayakubali madhehebu yote ya Kiislamu ya Kishia na Kisunni. Kwingineko mchambuzi mmoja wa kisiasa amesema magaidi wa Kitakfiri ambao wanatekeleza jinai kwa jina la Uislamu wanawasaidia wale wanaotaka kuuharibia jina Uislamu. Katika mahojiano na Press TV, Kevin Barret amesema makundi ya Kitakfiri yamewalipa pesa vijana Waislamu ambao hawajapevuka kiakili. Amesema mtandao wa al-Qaeda unaodai kufuata Uislamu una uungaji mkono mdogo sana katika ulimwengu wa Kiislamu. Barret amesema kuwa Uingereza ilishirikiana na Mawahhabi wa Saudia kuanzisha makundi ya Kitakfiri. Ametoa mfano wa kundi la kitakfiri la Boko Haram la Nigeria ambalo linachafua sura ya Uislamu kwa kuharamisha elimu.  Inafaa kuashiria hapa kuwa Mawahhabi wakufurishaji yaani Matakfiri wanaamini kuwa tafsiri yao ya Uislamu ndio sahihi na kwamba eti Waislamu wengine wote ni makafiri.

1406258

captcha