Akizungumza Jumatatu jioni mjini Tehran alipokutana na viongozi wa ngazi za juu wa mfumo na maafisa wa ngazi za juu wa majeshi nchini Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameeleza unyama wa Marekani ikiwa ni pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa mbwa mwitu Saddam Hussein dhidi ya Iran, shambulio dhidi ya ndege ya abiria ya Iran na mauaji ya halaiki ya mamia ya wanawake na watoto wasio na hatia waliokuwa katika ndege hiyo, mauaji ya mamia ya maelfu ya wananchi wa Iraq na Afghanistan na kuanzisha migogoro iliyosababisha umwagikaji damu katika nchi mbalimbali za duniani na kusisitiza kwamba, Wamarekani hawathamini maisha ya watu, amani na utulivu kwa wananchi wa maeneo mbalimbali duniani, na kamwe hawasiti kufanya shambulio la kijeshi kwa ajili ya kulinda maslahi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kadhia ya nyuklia hapa nchini ni nyeti mno hivyo haitaweza kufumbiwa jicho na wananchi wa Iran. Ayatullah Khamenei ameelezea matamshi yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa Marekani juu ya uwezekano wa kuendelezwa vikwazo dhidi ya Iran hata kama yatafikiwa makubaliano ya nyuklia na kusisitiza kwamba, kadhia ya nyuklia ni kisingizio tu na hata kama isingekuwepo, kungeibuliwa masuala mengine kama eti ukiukaji wa haki za binadamu, haki za wanawake na mengineyo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, Iran haina pingamizi lolote na uwepo wa njia au vyombo maalumu vinavyozuia upatikanaji wa silaha za nyuklia na kuongeza kwamba, Marekani haipasi kuingiwa na hofu na wasiwasi kwa nchi nyingine kuhusiana na suala la kujipatia silaha za nyuklia, kwani yenyewe imeshawahi kuzitumia silaha hizo hatari na hivi sasa bado inaendelea kujilimbikizia maelfu ya mabomu ya atomiki.
Akizungumzia masuala ya kieneo hasa fitina kubwa iliyozushwa hivi karibuni nchini Iraq, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu wananchi wa Iraq wataweza kuzima njama na fitina hizo na kwamba wananchi wa eneo hili watazidi kupiga hatua siku hadi siku katika masuala ya kimaendeleo na kiroho.