Katika hotuba yake, ameashiria takwa la Wapalestina la kuondolewa mzingiro na kusema takwa hilo ni la haki na hakuna mwanaadamu anayeweza kulikataa. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa Wapalestina wana haki wanaposema kuwa kukubali tu usitishwaji vita ni jambo ambalo litaupa utawala wa Kizayuni wa Israel idhini ya kuendeleza jinai zaidi bila kuadhibiwa sambamba na kuendeleza mzingiro na mashinikizo zaidi dhidi ya Wapalestina Ghaza. Kiongozi Muadhamu amegusia suala la kuongezeka chuki dhidi ya Marekani kote duniani kutokana na watawala wa Washington kushiriki katika jinai za Israel huko Ghaza. Ameongeza kuwa, 'hakuna anayeweza kuwaondoa Wamarekani lawamani kutokana na kuhusika kwao katika jinai na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa kikafiri wenye sifa za mbwa mwitu, ghasibu, katili, na dhalimu wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza; kwa msingi huo, Marekani sasa iko katika nukta dhaifu duniani. Kwingineko katika matamshi yake, Ayatullah Khamenei amesisitiza umuhimu wa Iran kuwa na maingiliano na dunia nzima na wakati huo huo amesema Iran haiwezi kuwa na maingiliano na Marekani na Utawala wa Kizayuni. Ayatullah Khamenei ameashiria kuongezeka mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran licha ya kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja ya Tehran na Washington katika kadhia ya nyuklia tokea mwaka jana. Amesema kinyume na baadhi ya watu waliovyodhania, mazungumzo hayo hayajasaidia chochote. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, katika hali ya hivi sasa, yaani kuendelea uhasama wa Marekani na matamshi ya kiuadui ya Kongres ya Marekani na wakuu wa serikali Washington dhidi ya Iran, hakuna msingi wa kuwa na mahusiano na Marekani. Akiwahutubia wanadiplomasia hao wa ngazi za juu Iran, Kiongozi Muadhamu amesema kuna haja ya kuwepo udiplomasia 'erevu na wenye harakati' katika kipindi hiki cha mpito cha kuelekea mfumo mpya duniani.