Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa PE, Waislamu hao wa nchini Marekani wameanzisha harakati za kuweka wazi milango ya misikiti kwa ajili ya watu wote wakati wa hafla zote zinazotekelezwa misikitini na katika vituo vyote vya Kiislamu chini ya usimamizi wa Baraza ka Kiislamu la California, lengo kuu likiwa ni kuutangaza Uislamu halisi unaopinga vitendo vya kigaidi na misimamo ya kufurutu ada. Mtandao huo wa habari umeandika kuwa, vituo vinne kati ya 27 vya Kiislamu vilivyoko mjini Inland, vitaanza kutoa huduma hiyo katika siku za Jumamosi na Jumapili wiki ijayo, kwa kuruhusu mtu yeyote mwenye maswali yake aende akaulize katika vituo hivyo na kupata majibu yanayouhusu Uislamu. Harakati hizo zinatazamiwa kutekelezwa pia katika miji mingine kama vile Riverside, Corona na Ontario katika jimbo la California huko Marekani. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni kundi la Waislamu wa mji wa Buffalo katika jimbo la New York iliwagawia wananchi wa mji huo mashada ya maua yenye semi na maneno ya Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mjumbe wa kundi la Jumuiya ya Waislamu wa mji huo (WNY) Samad Khan alinukuliwa akisema kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuhubiri utamaduni wa mazungumzo baina ya dini tofauti na kuanzisha anga ya kuwakutanisha pamoja wafuasi wa dini hizo kwa kutumia maua.../mh