IQNA

Kongamano la kimataifa la Kumtetea Mtume Mtukufu laanza Kuwait

16:10 - November 03, 2008
Habari ID: 1704103
Kongamano la pili la kimataifa la Kumtetea Mtume Mtukufu limeanza shughuli zake nchini Kuwait likisimamiwa na Wizara ya Waqfu na Masuala ya Kiislamu ya nchi hiyo.
Kongamano hilo la siku mbili linahudhuriwa na shakhsia na wasomi 400 wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali duniani ambao wanawakilishi Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Kimataifa ya Uislamu, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO, Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu, Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi na Benki ya Ustawi ya Kiislamu. Washiriki katika kongamano hilo watawasilisha makala na utafiti wao kuhusu nyanja za kibinadamu na kitamaduni za sira na mwenendo wa Mtukufu Mtume Muhammad SAW na mbinu mpya za kuchunguza sira ya Mtume kwa kuzingatia zama za sasa.
Kongamano hilo ambalo pia linahudhuria na wafuasi wa dini zisizokuwa za Kiislamu kutoka Ulaya na Marekani, kutakuwa pia na jukwaa la kutoa mafunzo ya kitaalamu na kuchunguza uzofu wa mipango ya huko nyuma kuhusu juhudi za kumtetea Mtume Mtukufu na kutathmini kiwango cha mafanikio yake.
Ajenda nyingine ya kongamano hilo ni pamoja na kuchunguza njia za kimatendo za kutetea sira na mwenendo wa Mtume SAW dhidi ya makundi yenye fikra za kufurutu mipaka ya Magharibi na kuchunguza mipango ya Jumuiya ya Kimataifa ya Kumtetea Mtume katika nchi zisizokuwa za Kiislamu.
Katika upande mwingine Mufti wa Misri Ali Juma amezitaka jumuiya na taasisi za Kiislamu kuungana na kushikamana kwa ajili ya kumtetea Mtume Muhammad SAW na kubuni njia za kuzuia vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu na itikadi za Kiislamu. 314314
captcha