IQNA

Palestina yapongeza marufuku ya Ireland kwa bidhaa zitokazo makazi Haramu ya Wazayuni

10:33 - July 27, 2026
Habari ID: 3482544
i
IQNA – Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imekaribisha hatua ya Ireland kutunga sheria inayopiga marufuku uagizaji wa bidhaa kutoka katika makazi haramu ya Kizayuni yaliyoko katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel, huku ikizitaka nchi na mabunge duniani kuchukua hatua kama hiyo.

Sheria hiyo ilitiwa saini na Rais wa Ireland, Catherine Connolly, na kukamilisha taratibu zote za kikatiba zilizohitajika ili kuanza kutumika rasmi.

Wizara hiyo imesema kuwa hatua hiyo ni maendeleo muhimu yanayoendana na juhudi za kidiplomasia za Palestina za kukata njia za msaada kwa mradi haramu wa makazi ya utawala wa Kizayuni, na kwamba inaakisi kujitolea kwa Ireland kwa misingi ya sheria ya kimataifa na uadilifu wa kimataifa.

Aidha, wizara imesisitiza kuwa utekelezaji wa sheria ya kimataifa ni wajibu wa kisheria unaozilazimu nchi kutoutambua wala kuusaidia uhalisia haramu ulioundwa na ukaliaji wa Kizayuni na shughuli za makazi haramu, ikiwemo kupitia shughuli za kibiashara, kiuchumi, kifedha, uwekezaji, na huduma zinazohusishwa na makazi hayo haramu.

Wizara hiyo pia imezitaka nchi, mabunge na watunga sheria kote ulimwenguni kufuata mfano wa Ireland kwa kuimarisha mifumo ya uwajibikaji wa kimataifa na kuweka vikwazo dhidi ya mradi haramu wa makazi ya Kizayuni, walowezi wavamizi wa Kizayuni, na yale iliyoyataja kuwa ni makundi yao ya kigaidi.

Sheria hiyo ilianza kutumika baada ya Rais Connolly kuitia saini tarehe 23 Julai, kufuatia kupitishwa kwake na bunge la chini tarehe 7 Julai na Seneti tarehe 15 Julai.

3498426

captcha