Mkutano huo uliandaliwa baada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti Mkuu wa al-Quds mjini Baghdad.
Wazungumzaji katika mkutano huo walisisitiza umuhimu wa mshikamano wa Kiislamu pamoja na mhimili wa fikra ya Husseini dhidi ya madhalimu wa dunia.
Sayyed Abdul Qadir Alusi, mkuu wa Jamiat Ulama ya Ribat Muhammadi nchini Iraq, katika hotuba yake alisisitiza umoja wa wanazuoni wa Kiislamu kutoka mataifa yote, akasema: “Misingi yetu ya kifikra na harakati ya wanafikra na wanazuoni wa Kiislamu lazima ijengwe juu ya mhimili wa umoja na mshikamano, na hili ni jambo lenye ulazima zaidi kuliko mengine yote katika mazingira ya leo ya ulimwengu wa Kiislamu.”
Aliongeza: “Tuna Qur’ani mmoja, Mtume mmoja, Qibla kimoja. Basi jambo linalopaswa kuwa kipaumbele cha kwanza katika ajenda ya wanazuoni wa Iraq, Iran, Lebanon, Misri na nchi zote, na wa madhehebu yote kuanzia Hanbali, Shafi’i, na pia makundi yote ya Wakurdi, Waturkmeni na wengineo, ni mshikamano na muqawama dhidi ya maadui wa Uislamu.”
Mwanazuoni huyo wa Kisunni amesema kuwa iwapo mshikamano wa Kiislamu uliosisitizwa na Qur’ani Tukufu na Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) utadhoofika, basi nguvu za kibeberu zitaelekea kuudhoofisha Uislamu, zitadhuru kiini cha muqawama katika ulimwengu wa Kiislamu, na kudhoofisha Umma wa Kiislamu.
Aliendelea kusema kuwa muqawama daima katika historia na pia katika zama za sasa umezunguka mhimili muhimu, na kwamba viongozi na makamanda wa muqawama wa Kiislamu, kuanzia Abu Mahdi al-Muhandis hadi Sayyed Hassan Nasrallah, kutoka Shahidi Soleimani hadi kwa viongozi mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wote waliuzunguka mhimili huo katika harakati zao; nao ni shakhsia na msimamo wa Imam Hussein (AS).
Ayatullah Ahmad Molabghi, mjumbe wa Baraza la Wataalamu la Iran, alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wengine katika mkutano huo.
Alisema kuwa umoja wa Umma ndio msingi wa kuthibiti kwa umoja wa ibada.
Ayatullah Molabghi aliongeza kuwa kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, Umma wa Kiislamu si dhana ya kiakili tu wala si wazo la kinadharia lisilo na uhalisia; bali ni ukweli wa kijamii na wa kihistoria.
“Vilevile, Qur’ani haisimamishi umoja katika kiwango cha chini. Umoja wa kabila, umoja wa dini, umoja wa kundi au wa harakati, japo waweza kuwa na thamani yake, lakini si upeo wa mwisho unaotakiwa na Qur’ani.”
Aliongeza kuwa Qur’ani inataka umoja uwe sifa ya Umma mzima, si sifa ya sehemu moja ya Umma dhidi ya sehemu nyingine.
Aidha alisisitiza kuwa Umma ama uwe na umoja na hivyo kuwa na nguvu, au utumbukie katika mzunguko wa migogoro na hatimaye kupoteza polepole mtaji wake wa kuwepo.
3498406