Akiwa na uso wa uthabiti na sauti iliyobeba athari ya miongo mingi ya kuandamana na Qur’ani Tukufu, alisimama kwenye jukwaa la “Dawlat al-Tilawa” akiwa na umri wa miaka 87 ili kusisitiza kuwa kuhifadhi na kufundisha Qur’ani hakufungwi na umri, na kwamba watu wa Qur’ani wataendelea kuwa chemchemi ya kuigwa na ya kutia ilhamu, kwa mujibu wa Al-Masrawy.
Al-Faradi, ambaye anatoka Abu Homs katika mkoa wa Bahira nchini Misri, alipata utambuzi maalumu kutoka kwa jopo la majaji wakati wa ushiriki wake katika kipindi hicho, na akapewa muda wa ziada, huku majaji wakisifu umahiri wake katika ahkam za usomaji wa Qur’ani na ubora wa utendaji wake.
Vilevile, waliwahimiza washiriki kunufaika na tajriba ya qari huyo wa Kimisri katika usomaji wa Qur’ani, jambo linaloakisi hadhi yake ya kielimu na historia yake ndefu ya kulitumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Safari ya Qur’ani ya Al-Faradi haikuwa nyepesi. Alikulia katika hali ya uyatima, na mazingira yake yakamlazimisha kufanya kazi ya kilimo tangu utotoni, hali iliyochelewesha hifdh yake ya Qur’ani. Hata hivyo, kadiri miaka ilivyokwenda, alifanya uamuzi uliobadili maisha yake: akaifanya Qur’ani kuwa njia yake na mwenendo wake wa maisha, na akajitolea kwa kuhifadhi, kusoma na kutadabbari aya za Mwenyezi Mungu.
Mmisri huyo hakusimama kwenye kuimudu tajwid na usomaji pekee, bali pia alijifunza elimu za Qur’ani, kanuni za tajwid, na qiraat mbalimbali za Qur’ani. Alikuwa akitumia takriban saa sita kila siku kwa ajili ya muraja’a na tilawa ya Qur’ani hadi akawa mmoja wa walimu mashuhuri zaidi wa Qur’ani katika Abu Homs.
Alifungua madrasa ya kuhifadhisha Qur’ani kwa watoto katika mtaa wake kwa ada ndogo, na pia akawa imam wa swala ya jamaa katika Msikiti wa Al-Tahrir huko Abu Homs.
Kwa miaka mingi, alifaulu kulea vizazi vya wasomaji wa Qur’ani, na kuwafundisha wengine wengi kusoma na kuandika.
Qari huyo wa Kimisri alipata umaarufu kwa sauti yake yenye mvuto na kwa uimara wake katika kanuni za usomaji wa Qur’ani.
Amesema kuwa ushiriki wake katika kipindi hicho cha televisheni ulitokana na kutiwa moyo na mwanafunzi wake, Sheikh Ahmed Amer, aliyemfahamisha kuwa usajili wa programu hiyo ulikuwa umefunguliwa. Hivyo aliamua kujipima katika mashindano hayo licha ya kushindana na washiriki waliokuwa na umri mdogo kwa miongo kadhaa kumshinda.
Al-Faradi ameeleza kuwa msomaji marehemu Sheikh Mustafa Ismail ndiye qudwa yake katika ulimwengu wa qiraat, kutokana na mtindo wake wa kipekee na madrasa yake ya Qur’ani ambayo imeathiri vizazi vya wasomaji.
Kuwepo kwa Al-Faradi katika programu ya “Dawlat al-Tilawa” kulizusha wimbi la fahari miongoni mwa watu wa mkoa wa Bahira, hasa wakazi wa Abu Homs na wanafunzi wake, ambao walitoa wito wa kuandaliwa hafla maalumu kwa ajili yake katika Msikiti wa Al-Tahrir, msikiti mkubwa zaidi katika eneo hilo, kama ishara ya kuthamini miongo yake ya kujitolea kufundisha Qur’ani.
Inafaa kutajwa kuwa msimu wa pili wa programu ya “Dawlat al-Tilawa”, ulioanza nchini Misri wiki chache zilizopita, unaendelea kugundua na kukuza vipaji vya wasomaji wa Qur’ani kutoka mikoa mbalimbali ya Misri.
Programu hiyo inatayarishwa kwa ushirikiano na Wizara ya Awqaf pamoja na Kampuni ya Al-Mutahidah Media Services, kwa lengo la kuwasaidia wahifadhi wa Qur’ani na kueneza utamaduni wa usomaji sahihi kwa mujibu wa kanuni za tajwid.
3498408