IQNA

Kurekodiwa Qiraa ya Tartil kulikuwa hatua muhimu katika khidma kwa Qur’ani

15:56 - July 26, 2026
Habari ID: 3482539
m
IQNA – Wizara ya Awqaf ya Misri imeadhimisha kumbukumbu ya kukamilika kwa rekodi ya kwanza ya kisomo au qiraa ya Tartil ya Qur’ani Tukufu mnamo Julai 23, 1961.

Wizara hiyo imesema katika taarifa kuwa mradi huo ulikuwa ni hatua ya kihistoria na yenye umuhimu mkubwa katika kuihudumia Qur’ani Tukufu na kueneza ujumbe wake kote duniani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi huo ulitekelezwa wakati huo chini ya usimamizi wa Wizara ya Awqaf kupitia Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Misri, na uliwezesha kufunguliwa kwa upeo mpya katika kufundisha na kueneza Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa ushirikiano na kundi la wanazuoni mashuhuri wa taaluma ya qiraat.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa mradi huo ulikuwa tunda la juhudi za Sheikh Mahmoud Shaltout, aliyekuwa Sheikh wa Al-Azhar wakati huo, pamoja na Labib Al-Said, aliyetoa wazo la kukusanya sauti ya usomaji wa Qur’ani kwa mfumo wa kurekodiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sheikh Mahmoud Khalil Al-Husari alichaguliwa kurekodi kisomo hicho cha Qur’ani kwa riwaya ya Hafs kutoka kwa Asim, chini ya usimamizi wa kamati maalumu ya kielimu na kitaaluma.

“Hatua hii imekuwa marejeo makuu ya sauti katika usomaji wa Qur’ani, na inasaidia kuhifadhi kisomo sahihi cha Qur’ani Tukufu na kupambana na majaribio ya kuipotosha. Aidha, inaakisi nafasi ya  Misri katika kuihudumia Qur’ani Tukufu kote duniani.”

Wizara hiyo imehitimisha kwa kusisitiza kuendelea kwa jitihada zake za kuihudumia Qur’ani kupitia mipango na miradi kadhaa, hasa mashindano ya televisheni ya “Dawlat Tilawa”, uendelezaji wa vituo vya mafunzo ya qiraat, pamoja na kuandaa mashindano ya Qur’ani yanayolenga kuimarisha hadhi ya Qur’ani nchini humo.

Inafaa kutajwa kuwa Sheikh Mahmoud Khalil Al-Husari ni miongoni mwa maqari wakubwa na mashuhuri wa Misri, aliyekuwa na sifa kadhaa za kipekee zilizomtenganisha na wasomaji wengine maarufu wa Qur’ani.

Alikuwa qari wa kwanza kusoma Qur’ani kwa mfumo wa Tartil na kuirekodi katika kanda za sauti, na pia alikuwa msomaji pekee ambaye kisomo chake kizuri na chenye mvuto kilisikika hata katika Ikulu ya White House.

Al-Husari alikuwa akisoma Kalamu ya Mwenyezi Mungu kwa khushuu maalumu na uzuri wa kipekee, hali iliyopenyeza athari yake ndani ya nyoyo za wasikilizaji.

3498409

Habari zinazohusiana
captcha