IQNA

Awamu Mpya ya Muqawama: Hamas yaangazia mabadiliko katika Ukingo wa Magharibi

15:41 - July 26, 2026
Habari ID: 3482537
IQNA – Kuongezeka kwa operesheni za muqawama au mapambano ya ukombozi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel kunaakisi kushindwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuwazuia Wapalestina kusimama kutetea ardhi yao, haki zao, na maeneo yao matukufu.

Hayo ni kwa mujibu wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, ambayo imesema Jumamosi kuwa kasi inayozidi kuongezeka ya operesheni za muqawama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu inaonesha wazi kushindwa kwa majaribio ya utawala wa Kizayuni ya kuwatia Wapalestina chini ya uonevu na kuwakatisha tamaa wasitetee ardhi yao na maeneo yao matukufu.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya mapambano kati ya Wapalestina na walowezi wa Kizayuni pamoja na vikosi vya uvamizi karibu na Nablus siku ya Ijumaa kusababisha kuuawa kwa wanajeshi wawili wa utawala wa Kizayuni, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kizayuni: afisa mmoja wa jeshi la Kizayuni aliyekuwa akiongoza kikosi cha betri katika Battalion 411 ya Brigade ya 282 ya mizinga, na askari mmoja kutoka Battalion 8119 ya Brigade ya 16 ya Al-Quds.

Katika shambulio hilo, Wapalestina wanne waliuawa shahidi na wengine wanne wakajeruhiwa, watatu miongoni mwao wakiwa katika hali mahututi.

Kiongozi wa Hamas, Mahmoud Mardawi, amepongeza msimamo wa thabiti wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na juhudi zao za kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea kuongezeka yanayofanywa na vikosi vya uvamizi vya Kizayuni na walowezi dhidi ya wakazi na mali zao, hususan katika vijiji vinavyozunguka Nablus, eneo linalojulikana pia kama Jabal al-Nar.

“Kuongezeka kwa namna inayoonekana kwa operesheni za muqawama katika Ukingo wa Magharibi, zikiwemo hujuma za kuchoma kwa visu na mashambulizi ya risasi, pamoja na ushujaa wa vijana wa mapambano na wakazi wa vijiji imara katika kukabiliana na magenge ya walowezi, ni ushahidi wa kushindwa kwa majaribio ya utawala wa Kizayuni kuwatiisha watu wetu wenye izza, kuvunja irada yao, au kuwazuia kutetea ardhi yao, maeneo yao matukufu, na kuhifadhi heshima yao,” amesema Mardawi.

Mardawi amesema mafanikio ya operesheni za karibuni katika kuwaua na kuwajeruhi wanajeshi wa uvamizi wa Kizayuni na walowezi yanaonesha kuwa muqawama katika Ukingo wa Magharibi unaingia katika awamu mpya.

Ameelezea maendeleo hayo kuwa ni “dalili ya kweli kwamba volkano ya Ukingo wa Magharibi imeanza kuinuka kutoka majivuni ili kulipiza kwa utawala wa Kizayuni kwa jinai zote ilizowatendea watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Gaza, na katika ardhi yote ya Palestina.”

Afisa huyo wa Hamas pia ametoa mwito wa kuongezwa kwa uungaji mkono kwa vijiji na miji ya Kipalestina inayokabiliwa na mashambulizi ya walowezi, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mwamko na mshikamano wa wananchi ili kuwazuia walowezi na kuwalazimisha kusitisha hujuma zao.

3498418

captcha