Kongamano la kimataifa la Maadili Katika Jamii ya Kiislamu limeanza shughuli zake katika mji mkuu wa Bahrain, Manama likihudhuriwa na maulama na wanafikra wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali duniani. Kongamano hilo linasimamiwa na Waziri Mkuu wa Bahrain Khalifa bin Salman Al Khalifa.
Shirika rasmi la habari la Bahrain (BNA) limeripoti kuwa, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Bahrain Abdullah bin Khalid Al Khalifa amesema kuwa wanafikra na wasomi wanaohudhuria kongamano hilo watachunguza masuala yanayohusiana na maadili katika jamii ya Kiislamu. Al Khalifa amesema kuwa miongoni mwa malengo ya kongamano hilo ni kuimarisha mafunzo ya maadili kwa ajili ya mtu binafsi na jamii, kustawisha umoja kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali na kujiepusha na hitilafu za kimakundi.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Bahrain amesema, katika mkutano huo wa siku mbili wasomi na wanafikra watawasilisha makala katika nyanja za maadili bora katika jamii ya Kiislamu. 314949