Daniel Glaser, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Fedha ya Marekani amesema kuwa Marekani imeanza kutoa mafunzo kuhusiana na mfumo wa huduma za fedha na uwekezaji wa Kiislamu katika vitengo vya fedha na benki nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti la Kuwait la al-Qabas, Daniel Glaser amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa na viongozi wa Marekani ili kunufaika na uzoefu wa mfumo wa uwekezaji na huduma za fedha za Kiislamu katika sekta ya benki na huduma za fedha nchini Marekani na pia kukabiliana na mgogoro wa fedha unaoendelea hivi sasa nchini humo. Akikiri kuwa uwekezaji wa Kiislamu unaunda sehemu kubwa na muhimu katika sekta ya uwekezaji duniani, Glaser amesema kuwa Wizara ya Fedha ya Marekani itashirikiana kikamilifu na wanauchumi pamoja na wataalamu wa masuala ya kifedha wa Chuo Kikuu cha Howard ili kutekeleza kikamilifu mpango wa kutoa mafunzo ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu. Afisa huyo wa Marekani amesema kuwa ni kwa sababu hiyo ndipo kikaandaliwa kikao cha kuzungumzia uwekezaji wa Kiislamu katika chuo hicho, kikao ambacho kinatazamiwa kuwakutanisha wanauchumi mashuhuri wapatao 100. Mwishoni Glaser amesema kuwa wanauchumi mashuhuri akiwemo Stuart Levey, Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani watahutubia kikao hicho. 318785