IQNA – Mtandao wa Mazungumzo ya Kiislamu nchini Norway ulishiriki katika “Arendalsuka,” ambayo ni jukwaa la kila mwaka la mijadala ya umma nchini Norway. Katika jukwaa hilo, mtandao huo ulijadili masuala muhimu ikiwemo utambulisho wa kidini, uhuru wa kujieleza, ubaguzi, na tofauti iliyopo kati ya ukosoaji halali wa dini na chuki zinazolenga jamii nzima.
Wawakilishi wa mtandao huo walisisitiza jukumu la taasisi za kidini katika kuimarisha mshikamano wa kijamii, wakibainisha kuwa kupambana na msimamo mkali na chuki kunahitaji mazungumzo na ushirikiano kati ya wadau mbalimbali katika jamii.
Mijadala hiyo pia ilijikita katika changamoto zinazowakabili vijana wa Kiislamu nchini Norway, ikiwemo dhana potofu, ubaguzi, na changamoto za kujieleza kwa utambulisho wao wa kidini na kiutamaduni.
Katika paneli iliyopewa kichwa cha “Wakati Chuki dhidi ya Makundi Inajificha kama Ukosoaji wa Kidini,” washiriki walisisitiza tofauti iliyopo kati ya kukosoa imani za kidini na usemi unaogeuka kuwa ubaguzi au uchochezi dhidi ya jamii fulani.
Mtandao wa Mazungumzo ya Kiislamu wa Norway pia uliainisha umuhimu wa taasisi za kidini kama washirika wa kijamii katika kuzuia msimamo mkali, kupunguza migawanyiko ya kijamii, na kuchangia katika usalama na mshikamano katika jamii ya Norway.
Kwa mujibu wa mtandao huo, wanachama wengi wa kamati walisisitiza kuwa taasisi za kidini hazijikiti tu katika kutoa nafasi za ibada, bali pia zinatumika kama washirika wa kimkakati katika juhudi za kuimarisha usalama na mshikamano wa kijamii.
Mtandao wa Mazungumzo ya Kiislamu unatumika kama mfumo wa kijamii unaolenga kukuza mazungumzo ya kidini na ya kiutamaduni, pamoja na kuimarisha maadili ya uelewa na kuishi kwa amani ndani ya jamii za Ulaya.
3498662