IQNA

17:01 - August 16, 2026
Habari ID: 3482634

Mwanazuoni wa Iran atoa wito wa Akili Mnemba (AI) kuwa chachu ya mageuzi katika taaluma za Qur’ani

IQNA – Mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Iran ametoa wito wa kuitumia Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) siyo kama nyenzo ya kusaidia pekee, bali kama chachu kuu ya kuleta mageuzi katika tafiti na harakati za Qur’ani.

 Ebrahim Ebrahimi

Hujjatul Islam Ebrahim Ebrahimi, Mkuu wa Kituo cha Kuratibu Utafiti wa Qur’ani, Elimu ya Juu, na Sayansi ya Jamii cha Iran, aliyasema hayo katika kikao cha Jumamosi cha Kikundi Kazi cha Teknolojia Mpya na Akili Mnemba, kilichopo chini ya Tume ya Maendeleo ya Utafiti na Elimu ya Juu ya Qur’ani Iran.

Hujjatul Islam Ebrahimi alielezea mpango huo kama “dhamira ya kitaifa na ya kisekta,” akisisitiza kuwa matumizi ya AI katika mambo ya Qur’ani yasichukuliwe kama mradi wa utafiti au teknolojia pekee.

Alisema dhamira hiyo, ambayo imeelekezwa na Baraza la Maendeleo ya Utamaduni wa Qur’ani, inahitaji ushiriki wa dhati wa taasisi za serikali, vyuo vikuu, vituo vya utafiti, na taasisi za Qur’ani kote nchini.

Katika miaka ya hivi karibuni, Hujjatul Islam Ebrahimi alisema kuwa AI kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichukuliwa kama nyenzo ya kuunga mkono elimu na utafiti. Hata hivyo, alitoa wito wa kubadili mtazamo huo.

“Leo, ni lazima tuinue fikra zetu na kuichukulia Akili Mnemba kama moja ya vichocheo vya mageuzi katika nyanja ya tafiti na harakati za Qur’ani,” alisisitiza.

Alihimiza vikundi kazi vya utafiti, elimu, mambo ya kimataifa, na sayansi ya binadamu ya Qur’ani kuikumbatia teknolojia hii na kusaidia kuibua mbinu za kutumia uwezo wake ipasavyo.

Wakati huohuo, Hujjatul Islam Ebrahimi alichora mstari bayana kati ya msaada wa kiteknolojia na mchakato wa kuielewa misingi ya Wahyi.

“Hatuna nia ya kukabidhi ufahamu wa Qur’ani Tukufu kwa Akili Bandia,” alifafanua. “Ufahamu wa Qur’ani unategemea elimu ya msingi (maarifah), fiqhi, tafsiri, na uelewa wa kitaaluma; na Akili Bandia haiwezi kuchukua nafasi ya wafasiri, watafiti wa Qur’ani, na wanazuoni katika fani hii.”

Aliongeza kuwa lengo ni kuitumia AI kama nyenzo madhubuti ya kuunga mkono uelewa wa kina wa Qur’ani, kupanua wigo wa utafiti wa Qur’ani, kurahisisha upatikanaji wa rasilimali za kielimu, na kuinua ubora wa elimu ya Qur’ani.

3498666

Habari zinazohusiana
captcha