IQNA

Wanafunzi wa Gaza Wahitimisha Kusoma Qur’ani Nzima Katika Kikao Kimoja

17:47 - August 04, 2026
Habari ID: 3482585
IQNA-Katika mwendelezo wa kuonyesha ustahimilivu na ari ya kiimani katikati ya mapambano, wanafunzi 110 wa kike wenye kuhifadhi Qur’ani huko Gaza wamefanikiwa kuhitimisha usomaji wa Qur’ani nzima katika kikao kimoja cha Khatm al-Qur’an.

Tukio hili la kipekee liliadhimishwa na Idara ya Awqaf ya Gaza kwa kushirikiana na Taasisi ya Misaada ya Kibinadamu (IHH), likiwa ni ushahidi wa nguvu ya roho za waumini zinazokataa kukata tamaa licha ya mashambulizi yanayoendelea. Wanafunzi hao, ambao wanatoka katika Idara ya Wanawake ya Kuhifadhi Qur’ani (Diwan al-Hafiz), walionyesha kiwango cha juu cha nidhamu na mapenzi kwa Kitabu kitukufu.

Tukio hilo lilikuwa sehemu ya Siku ya Qur’ani ya ‘Taratil al-Tamkeen’, programu ambayo imekuwa ikitekelezwa sambamba na mfululizo wa jitihada za Wizara ya Awqaf na Mambo ya Dini ya Ukanda wa Gaza katika kuhifadhi na kueneza mafundisho ya Qur’ani. Mohammed Salem, Mkurugenzi Mkuu wa Kurugenzi ya Qur’ani na Sunnah ya wizara hiyo, alipongeza hatua hiyo yenye baraka ambapo wanafunzi walihitimisha Qur’ani nzima katika kikao kimoja kwa mara ya kwanza. Katika maelezo yake yaliyojaa hisia, alielezea tukio hilo kama “chemchemi ya fahari na heshima kwa Gaza na watu wake,” akimshukuru Diwan al-Hafiz kwa kuandaa mazingira ambapo wanafunzi waliweza kuelekeza muda wao katika utumishi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Asaad al-Mushtahi, Mkurugenzi wa Idara ya Awqaf ya Gaza, alisisitiza kuwa azimio la wanafunzi hawa la kuhifadhi na kusoma Qur’ani, linaloendelea kwa nguvu licha ya vita na uharibifu, linatoa ujumbe mzito kwa ulimwengu mzima. Ujumbe huo ni kuwa watu wa Gaza wanaendelea kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu licha ya masaibu yote yanayowakabili. Ni wazi kuwa kwa wananchi hawa, kusoma na kuhifadhi Qur’ani si kitendo cha kawaida tu, bali ni msimamo wa kiroho wa kupinga dhulma.

Vikao hivi vya usomaji wa Qur’ani huko Gaza si jambo geni, hata katikati ya vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Kizayuni. Kabla ya tukio hili, wanafunzi wengine 105 walihitimisha Qur’ani nzima katika kikao kimoja ndani ya Msikiti wa Sayyid Qutb katika kambi ya Nuseirat. Waandaaji na washiriki wa tukio hilo walielezea furaha yao na azimio lisilotikisika la kuendeleza vuguvugu hili la Qur’ani, wakionyesha kuwa hata katika nyakati ngumu zaidi, nuru ya Qur’ani ndiyo inayowaongoza na kuwapa nguvu katika safari yao ya haki na ukombozi.

/3498521

 

Habari zinazohusiana
captcha