IQNA

Kuandaliwa kila mwaka mashindano ya Qur’ani kutayaimarisha

9:14 - November 13, 2008
Habari ID: 1707723
Kuandaliwa kila mwaka mashindano ya Qur’ani Tukufu ya wanachuo wa Kiislamu kutaleleta muamko na mvuto maalumu katika mashindano hayo na hivyo kuyaimarisha zaidi.
Jambo hilo litaandaa uwanja wa wanachuo zaidi kushiriki katika mashindano hayo na hivyo kupata uzoefu zaidi kuhusiana na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Hayo yamesemwa na Hassan Abubakr, mwanachuo raia wa Ghana ambaye yuko katika mwaka wa mwisho wa masomo yake ya juu humu nchini. Amesema, namna ya upashaji habari kuhusiana na mashindano hayo ya Qur’ani ya wanachuo wa Kiislamu si ya kuridhisha na kwamba viongozi wa Iran wanapasa kufanya juhudi zaidi ili kuimarisha njia za upashaji habari duniani kuhusiana na mashindano hayo ili wanafunzi wengi zaidi wapate kushiriki. Ameongeza kuwa bila shaka kushiriki kwa idadi kubwa ya wanachuo wa Kiislamu katika mashindano hayo kutafanya idadi kubwa ya wanachuo kutoka nchi mbalimbali kuja humu nchini na kujionea wenyewe kwa karibu maendeleo ya Iran katika Nyanja mbalimbali zikiwemo za Qur’ani na hivyo kupunguza athari na propaganda mbaya inayoenezwa ulimwenguni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hassan Abubakr amesema kuwa mashindano ya Qur’ani ya wanachuo wa Kiislamu yanayoandaliwa na Iran yana athari kubwa katika kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu, kwa sababu watu wanaoshiriki katika mashindano hayo hawaji nchini kwa ajili ya mashindano hayo tu bali ni kwa ajili ya kujua Uislamu ulivyo nchini Iran na pia kuifahamu zaidi Iran ya Kiislamu. Amesema Waislamu wanaoshiriki katika mashindano hayo hujuana na kuanzisha uhusiano wa kirafiki na kidugu. Hassan Abubakr ameongeza kuwa kuhudhuria shakhsia na wasomaji mashuhuri wa Qur’ani katika mashindano ya mjini Tehran ni nukta nzuri na ya kuvutia kwa sababu jambo hilo linawashawishi na kuwashajiisha wasomaji wanaoinukia waweze kufanya jitihada zaidi za kusoma na kukifahamu vyema kitabu hicho na mbinu mbalimbali za kukisoma kwa lahani za kuvutia. Amesisitiza kwamba haitoshi kwa msomaji wa Qur’ani kukisoma kitabu hicho cha mbinguni kwa sauti nzuri tu bali anapasa kuzingatia kila neno analolisoma katika kitabu hicho ili kupata maana yake halisi na hivyo kuweza kumuathiri maishani. Amemaliza kwa kusema kuwa kwa bahati mbaya Waislamu wamepuuza na kuyapa umuhimu mdogo maneno yaliyomo katika kitabu hicho, jambo linalowafanya Wamagharibi walio na uadui mkubwa dhidi ya Uislamu na Waislamu kuyatumia dhidi yao. 319426
captcha