Gazeti la Saudi Arabia la al-Watan limeandika kuwa katika sherehe hizo, maimamu wa sala ya jamaa wa kituo hicho ambao walikuwa wa kwanza kuwahi kusajiliwa katika mfumo wa masomo ya kituo hicho cha Kiislamu walitunukiwa shahada za kuhitimu masomo na loho za shukrani. Wahitimu hao ambao watatu miongoni mwao ni wanawake wamesoma katika Kituo cha Kiislamu cha al-Ghazali kwa muda wa miaka minne na pia kujifunza masuala yanayohusiana na sheria za kiraia na za Ufaransa katika Taasisi ya Kanisa Katoliki ya mjini Paris. Katika sherehe hizo, wanafunzi kadhaa wakiwemo mabinti tisa wamepewa vibali vya kuendesha shughuli za uhubiri wa Kiislamu nchini Ufaransa. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Masuala ya Ndani ya Ufaransa, kuna maimamu wa swala ya jamaa wapatao 2000 wanaojishughulisha na swala za jamaa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo ni nusu tu ya maimamu hao ndio wanaozungumza lugha ya Kifaransa na asilimia 20 kati yao ni wenye asili ya Ufaransa. Kuna misikiti na sehemu za kuswalia zipatazo 1890 nchini Ufaransa na Uislamu ndiyo dini ya pili kwa ukubwa baada ya Ukristo kwa kuwa na wafuasi zaidi ya milioni tano. 324374