Nidhal Ammar, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanachuo wa Kiarabu amesema kwamba mwanachuo wa Kiislamu amebeba ujumbe wa amani kwa Walimwengu. Ameyasema hayo alipozungumza katika mahojiano maalumu na Shirika la Habari za Qur’ani la Kimataifa IQNA na kuongeza kuwa, wanachuo wa Kiislamu wana nafasi muhimu katika zama hizi.
Amesema, wameweza kufikia ngazi muhimu za kielimu na kiutafiti na kwamba Ulimwengu wa Kiislamu unaweza kuwategemea katika kuleta maendeleo na ustawi. Amebainisha ujumbe wa wanachuo wa Kiislamu katika kupambana na hujuma ya nchi za Magharibi na kusema kuwa, wanachuo hao wamebebea ujumbe wa amani na mapenzi kwa walimwengu na kwamba kwa kuzingatia mafundisho ya Kiislamu na maadili, wanaweza kutoa mfano mzuri na wa kuigwa na walimwengu.
Huku akibainisha kwamba nchi za Magharibi huwanasibisha Waislamu na kila aina ya ugaidi unaotekelezwa katika pembe mbalimbali za dunia, Ammar amesisitiza kuwa huo ndio mtazamo potofu unaotawala katika fikra za watu waliowengi wa nchi za Magharibi. Amesema, ili kuondoa picha hiyo potofu Waislamu wanapasa kufanya juhudi maradufu huku wakizingatia umuhimu wa umoja miongoni mwao. Ammar pia amesema kuwa vikao na makongamano ya Kiislamu yanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuvunja njama za Wamagharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Amesema mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Waislamu yana nafasi muhimu katika kutatua matatizo yao. Ammar amesema mwishoni mwa mazungumzo yake kwamba, jumuiya ya kimataifa ya wanachuo wa Kiislamu inapasa kuasisiwa ili kueneza zaidi thamani za Kiislamu ulimwenguni. 327699