IQNA

Uadilifu na amani, msingi wa uhusiano wa mataifa ulimwenguni

10:50 - December 04, 2008
Habari ID: 1715745
Washiriki wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa 'mazungumzo kati ya Uislamu na Ubudha' nchini Singapore wametoa taarifa mwishoni mwa kikao chao hapo Jumanne tarehe Pili Disemba wakisema kwamba, uadilifu, amani na urafiki ni miongoni mwa misingi muhimu ya uhusiano wa mataifa, wafuasi wa dini na tamaduni mbalimbali duniani.
Maudhui muhimu ya mkutano huo uliodhaminiwa na Jumuiya ya Uhubiri wa Kiislamu nchini Singapore ilikuwa ni 'Amani, urafiki na thamani za dunia.' Hamid bin Ahmad ar-Rifai, Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mazungumzo ya Kiislamu, na idadi kadhaa ya viongozi wa Kibudha kutoka nchi za China, Singapore, Cambodia, Thailand, Ufilipino, Malaysia. Indonesia na Taiwan wameshiriki katika mkutano huo. Taarifa ya mwisho ya mkutano huo ilitaka kuheshimiwa matukufu ya dini na kutekelezwa miradi ya pamoja kwa ajili ya kueneza thamani za uadilifu, amani na kuheshimiana duniani. Washiriki wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa kufanywa vikao na mikutano ya pamoja, kuimarishwa mazungumzo miongoni mwa viongozi wa kidini za Kiislamu na Kibudha, pamoja na kuandaliwa duru za mafunzo kwa ajili ya kueleweka vyema misingi na mafundisho ya dini hizi. Ar-Rifai amesema kuwa, dini mbili hizi zina misingi yenye thamani kubwa kwa jamii ya mwanadamu na kutaka kuimarishwa mazungumzo ya pande mbili na vilevile kuheshimiana wafuasi wa dini hizi. 329312
captcha