Ayatullah Taqi Mudarrisi, mmoja wa maraaji' wa Kishia wa nchini Iraq amesema kuwa msimu wa hija ni fursa nzuri kwa Waislamu kuimarisha thamani za Kiislamu na ujumbe wa Ahlul Beit (as) katika jamii za Kiislamu, na wakati huohuo kutahadharisha dhidi ya kufutwa utambulisho wa Kiislamu na kudhoofishwa nara za Waislamu.
Katika ujumbe alioutoa kwa Waislamu kupitia televisheni ya satalaiti ya Ahlul Beit ya nchini Iraq, Ayatullah Mudarrisi amewataka Waislamu wote wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba kutumia fursa hiyo ili kunufaika kimaanawi na amali za hija. Amesema kuwa, msimu wa hija ni fursa nzuri kwa mwanadamu kufanya juhudi za kukosha roho yake na kusisitiza kuwa, amali za hija zina athari kubwa katika maisha ya mwanadamu. Amesema athari hizo huweza kuonekana mara moja katika tabia na maisha ya mtu binafsi na kijamii ya mahujaji. Katika kuendelea na ujumbe huo, Ayatullah Mudarrisi amewataka Waislamu kuitazama hija kama amali ya kiustaarabu na kuichukulia kuwa fursa ya kulinda utambulisho wao wa Kiislamu na pia kuimarisha thamani za Kiislamu na Ujumbe wa Ahlul Beit (as) katika jamii zao. Amesema mwishoni mwa ujumbe huo kwamba, kuimarishwa kwa thamani hizo katika jamii huleta msisimuko na uchangamfu katika umma wa Kiislamu, kama ambavyo upuuzaji wake hufuta utambulisho wa Kiislamu na kuufanya uyeyuke na kumezwa na tamaduni nyinginezo. 332088