Kikao cha tano cha pamoja cha Kituo cha Mazungumzo ya Dini cha Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu na Baraza la Kimataifa la Makanisa, kilianza jana Jumamosi hapa mjini Tehran chini ya anwani ya 'Dini na Maisha ya Amani.'
Kikao hicho cha kimataifa cha siku mbili kinahudhuriwa na wawakilishi wa Kiislamu na Kikristo kutoka nchi za Denmark, Uswisi, Marekani, Syria na Iran. Viongozi wa makanisa ya Iran pia wanahudhuria kikao hicho.
Katika kikao hicho kilichofunguliwa kwa kusomwa aya kadhaa za Qur'ani Tukufu na Injili, Rasul RasuliPur, Mkuu wa Kituo cha Mazungumzo ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Kubuni Siasa za Kidini la Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu alitoa hotuba ya kuwakaribisha wageni wanaohudhuria kikao hicho. Kikao hicho kimepangwa kujadili masuala mbalimbali yakiwemo ya dini, utamaduni na mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo, maisha ya amani kati ya Waislamu na Wakristo wa Ulaya, wafuasi wa dini za wachache na changamoto mbalimbali zinazowakabiliwa wafuasi wa dini mbili hizi muhimu.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Husseiniya ya Az-Zahra ya Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu. 333064