IQNA

Kunyamazia kimya jinai za Gaza ni sawa na kuziunga mkono

17:57 - December 20, 2008
Habari ID: 1720787
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naeem Qasim amesema kuwa kimya cha viongozi wa nchi za Kiarabu mbele ya jinai za Wazayuni huko Gaza ni sawa na kuunga mkono mzingiro wa adui anayekalia ardhi za Wapalestina kwa mabavu. Ametoa wito kwa Umma wa Kiislamu kufanya uwezalo kuwanusuru watu wa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IQNA tawi la Beirut, Sheikh Naeem Qasim ameyasema hayo Ijumaa alipohutubia hadhara kubwa katika maandamano yaliyofanyika kwa lengo la kutangaza mshikamano wa Lebanon na taifa linalodhulumika la Palestina. Sheikh Qasim amesema kuwa, kadhia ya Palestina ndiyo kadhia kuu kimataifa na kwamba Waislamu wanataka ardhi zote za Palestina zikombolewe kutoka kwenye makucha ya Wazayuni. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema:Vikao vya Baraza la Usalama kuhusu Ukanda wa Gaza vinafanyika kwa lengo la kufunika njama za Marekani na kuwasahaulisha walimwengu jinai za utawala wa Kizayuni.
Sheikh Qasim ameendelea kusema kuwa: “ Sisi tutabaki na Wapalestina hadi pale watakapopata uhuru kamili”. Aidha ametoa wito kwa serikali ya Misri kuchukua hatua ya kihistoria kwa kuwasaidia Wapalestina wanaoteseka huko Gaza.
Mamia ya maelfu ya Walebanon walijitokeza katika maandamano hayo ya mjini Beirut na kutangaza mshikamano wao na Wapalestina wanaoteseka katika Ukanda wa Gaza. Maandamano hayo yamefanyika kujibu wito wa Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah. Waandamanaji walikuwa wakitoa nara kama vile "Mauti kwa Israel" na " Mauti kwa Marekani" huku wengine wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa "Hapana kwa amani inayosababisha maafa ya kibinadamu" na "Mwenyezi Mungu amlinde kiongozi wetu Nasrullah".
Maandamano mengine yamefanyika kusini na kaskazini mwa Lebanon na vile vile katika Bonde la Bikaa.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina Ismail Haniyah amempongeza Sayyid Hassan Nasrallah kwa juhudi zake za kusimama bega kwa bega na Wapalestina huko Ghaza. Haniyah amesema maandamano makubwa yaliyofanyika huko Lebanon Ijumaa ni ishara kuwa ulimwengu wote umechoshwa na mzingiro wa Wazayuni huko Ghaza. 335825
captcha