IQNA

Tantawi anapaswa kunyamaza kimya badala ya kupayuka

15:50 - December 22, 2008
Habari ID: 1721654
Mhubiri wa Kiislamu wa Misri Ahmad al Mahlawi amekosoa mbinu inayotumiwa na Sheikh wa al Azhar Sayyid Muhammad Tantawi katika kuamiliana na masuala ya Waislamu akisema: Bora anyamaze kimya kuliko kupayuka.
Sheikh Ahmad al Mahlawi amenukuliwa na gazeti la Al Masri al Yaum akisema kuwa, mbinu inayotumiwa na Sheikh Tantawi katika kuamiliana na masuala na matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu haifai na inaamsha hasira na kuwachukiza Waislamu.
Amesema: Mwenendo na matamshi ya Tantawi yanachafua sura na nafasi ya maulama na wanafikra wa Kiislamu.
Amesema kuwa hashangazwi na matamshi ya Sheikh Tantawi, kwani kiongozi huyo wa al Azhar hana msimamo imara katika matamshi na maamuzi yake ya kidini na kisiasa.
Sheikh al Mahlawi ameongeza kuwa: Tantawi amekanyaga mistari yote myekundu baada ya kupeana mkono na Rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel Shimon Peres na kwamba ni aibu kwa kiongozi huyo kutokuwa na maarifa juu ya masuala muhimu yanayoukabili umma wa Kiislamu ukiwemo mzingiro wa utawala katili wa Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza.
Mhubiri huyo mashuhuri wa Kiislamu wa Misri amesisitiza kwamba, kitendo cha Tantawi cha kupeana mkono na Rais wa utawala ghasibu wa Israel na kutojali kwake hali na matatizo ya Waislamu ni jinai kubwa ambayo iwapo wanadamu hawawezi kuishughulikia, basi Mwenyezi Mungu (sw) hataicha siku ya Kiyama. 336184
captcha