Abdallah bin Abdul Muhsin at-Turki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu amesema kuwa, nchi za kibeberu duniani zikiongozwa na Marekani, ndio wahusika halisi wa mashambulio ya kinyama ya anga yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza.
Akitoa radiamali yake kuhusiana na mashambulio ya kinyama yaliyofanywa siku ya Jumamosi na utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza, at-Turki amesema kuwa Marekani na nchi nyingine za Magharibi ndio waungaji mkono wakuu wa mashambulio ya kinyama yanayofanywa mara kwa mara na Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina. Amesema kuwa hatua ya hivi karibuni ya askari jeshi wa utawala wa Kizayuni ya kuwaua kwa umati watoto na watu wa Gaza inakwenda kinyume kabisa na mafundisho ya dini zote za mbinguni pamoja na sheria za kimataifa. Amezitaka nchi za Kiislamu, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kufanya kila liwezekanalo kwa madhumuni ya kusimamisha mara moja mashambulio hayo ya Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia.
Katika taarifa aliyotoa kuhusiana na suala hilo, at-Turki amesema kuwa ulimwengu wa Kiislamu umeshangazwa mno na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuwashambulia kinyama wakazi wa Ukanda wa Gaza baada ya kuwazingira kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja, ambapo umezuia kabisa kuingizwa katika ukanda huo bidhaa muhimu yakiwemo madawa, maji safi ya kunywa, umeme na chakula. Amesema, mashambulio hayo yanathibitisha wazi uongo mkubwa wa Marekani na utawala wa Tel Aviv kuwa zinafuatilia amani ya kudumu katika eneo nyeti la Mashariki ya Kati.
Mwishoni at-Turki amelitaka Baraza la Usalama kusimamisha mara moja mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yanayozuia kivitendo kupatikana uthabiti na amani ya kudumu katika eneo hili muhimu kimataifa, na kuwawezesha Wapalestina kurudisha haki zao za kimsingi. 339713