IQNA

Bush aunga mkono jinai za Wazayuni, maandamano ya kulaani Wazayuni yaendelea duniani

11:02 - January 04, 2009
Habari ID: 1726877
Kwa mara nyingine Rais George Bush wa Marekani amesema bila ya aibu kwamba anaunga mkono kwa kila hali mashambulizi ya Utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza.
Rais huyo wa Marekani ameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua dhidi ya wanamapambano Waislamu wa harakati ya Hamas ili wasitishe hujuma yao ya makombora dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Bush amesisitiza kuwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni yatasimamishwa huko Gaza iwapo tu makundi ya mapambano ya Palestina yatajidhalilisha mbele ya Israel na kutii kila unachotaka utawala wa Kizayuni.
Mara baada ya Bush kutangaza uungaji mkono wake wa kila hali kwa jinai za Wazayuni, wakuu wa Israel wamepanda kichwa na kutangaza kuwa hawatakomesha mashambulizi yao dhidi ya Wapalestina.
Matamshi ya Bush yanakuja katika hali ambayo nchi mbalimbali duniani zilishuhudia maandamano makubwa dhidi ya Wazayuni baada ya swala ya Ijumaa. Polisi ya Misri imemtia mbaroni Mahmoud Izzat Katibu Mkuu wa kundi la Ikhwanul Muslimiin nchini Misri pamoja na viongozi wengine wa kundi hilo kwa kosa eti la kushiriki kwenye maandamano yaliyofanyika nchini humo kulani mauaji ya Gaza. Nchi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Morocco, Pakistan, Afghanistan, Tajikistan, Uingereza, Malaysia, Indonesia, Jordan, Ireland, Uturuki, Ufilipino, Mexico na nchi nyinginezo kadhaa za Ulaya, Afrika na Asia zimefanya maandamano zikilaani mauaji ya Israel huko Gaza.
Maandamano Afrika Mashariki kulaani Wazayuni
Huko Afrika Mashariki, mamia ya Waislamu waliandamana katika mji mkuu wa Tanzania Dar-es-Salaam kulaani jinai za Wazayuni huko Gaza. Maandamano hayo ya Ijumaa yalifanyika katika eneo la Kidongo Chekundu.
Akihutubia mkutano huo, Professor Haroub Othman wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam alisema: "Tunalaani mauaji ya Ghaza. Kwa miaka 60 Israel imekuwa ikipokea misaada ya kiuchumi na kijeshi kutoka Magharibi na hasa Marekani na hilo limeuwezesha utawala huo kuendeleza hujuma dhidi ya Wapalestina". Mhadhiri huyo maarufu wa Tanzania ametaka viongozi wa Israel wafikishwe mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kujibu mashtaka ya kuhusika na mauaji ya umati. Naye Prof. Issa Shivji vile vile wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ametaka wafuasi wa dini zote kuwaunga mkono Wapalestina.
Kwa upande wake mwanazoni mashuhuri wa Tanzania Sheikh Ali Basaleh ametoa wito kwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kutuma vikosi vya kulinda amani kuzuia hujuma ya Wazayuni Ghaza.
Katika nchi jirani ya Kenya, Waislamu pia waliandamana baada ya sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Jamia kati kati ya jiji la Nairobi na kutoa mwito kwa Rais Mwai Kibaki wa nchi hiyo kukata uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya Hassan Omar amesema hujuma ya Wazayuni huko Ghaza ni katika fremu ya njama za Wamagharibi za kuwakandamiza Waislamu. Aidha Waislamu nchini Kenya wamezilaumu balozi za nchi za Kiarabu mjini Nairobi kwa kutotoa taarifa yoyote ya kuwaunga mkono Wapalestina. Ni balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pekee, Bw. Hamid Moayyer, aliyelaani jinai za Wazayuni. Mbunge wa eneo la Kisumu Mashariki huko Magharibi mwa Kenya, Shakeel Shabir amesema atawahimiza Wabunge Waislamu kupitisha kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Moses Wetangula endapo hatalaani jinai za Wazayuni.
Wakati huo huo Waislamu wa Kenya wameapa kufanya maandamano mbele ya ubalozi wa utawala wa Kizayuni wakimtaka balozi huyo kuondoka nchini humo mara moja.
Katika mji wa pwani ya Kenya wa Mombasa Waislamu waliandamana Alhamisi kulaani jinai za Wazayuni na kutangaza kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa.
Maandamano yalianzia Msikiti wa Kwa Shibu eneo la Mwembe Tayari na kumalizikia viwanja vya Makadara paliposaliwa swala ya Jamaa. Maandamano hayo yaliongozwa na Sheikh Hassan Omar Mweka Hazina wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Kenya CIPK. Sheikh Omar alisema Waislamu wamekasirishwa na mauaji ya kinyama ya Wapalestina huko Ghaza. Aidha aliitaka serikali ya Kenya kufunga ubalozi wa utawala wa Israel mjini Nairobi. Waandamanaji hao walizichoma moto bendera za Marekani na utawala haramu wa Israel. 342823
captcha