IQNA

Baraza la Usalama litume ujumbe kusimamia usitishaji mashambulio ya Israel

9:47 - January 05, 2009
Habari ID: 1727593
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, wametoa taarifa mwishoni mwa kikao chao cha dharura huko Jeddah nchini Saudi Arabia wakilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutuma timu ya kusimamia usimamishaji mashambulio ya kinyama yanayofanywa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Taarifa hiyo imesema kuwa, kwa kutoa azimio lisilo la kuilazimisha Israel kusimamisha mashambulio yake dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza, Baraza la Usalama limekwepa jukumu lake zito la kulinda amani na usalama duniani. Kikao hicho cha Jeddah kimetaka kufanyika mara moja kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusimamisha mashambulio ya Israel dhidi ya watu wasio na hati huko Gaza na pia kuwataka mabalozi wa nchi za Kiislamu wanaohudumu mjini Geneva Uswisi kulifahamisha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini humo jinai na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala huo dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina.
Taarifa ya mawaziri hao imetaka kukomeshwa kwa hitilafu na mivutano ya makundi ya Palestina na kuimarishwa umoja miongoni mwao kwa madhumuni ya kukabiliana na hujuma ya kinyama ya Wazayuni dhidi yao. Wametaka kufunguliwa kwa vivuko vyote vya Gaza ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kutoka katika nchi za Kiislamu kupelekewa watu wanaoihitajia.
Pamoja na kuwa zaidi ya wiki moja imepita sasa tokea kuanzishwa kwa mashambulio ya kinyama ya Wazayuni dhidi ya wakazi wasio na ulinzi wa Gaza, lakini Umoja wa Nchi za Kiislamu sawa na taasisi nyingine za kimataifa, haujachukua hatua yoyote muhimu ya kuzuia mashambulio hayo, na bila shaka kutolewa taarifa tu bila ya hatua za kivitendo hakutasaidia kutatuliwa kwa machungu na masaibu yanayowapata wakazi wa Ukanda wa Gaza. 343515
captcha