IQNA

Taarifa ya Kituo cha Kiislamu cha Uingereza yaalani jinai za Israel

9:34 - January 12, 2009
Habari ID: 1729597
Kituo cha Kiislamu cha Uingereza kimetoa taarifa kikilaani vikali jinai na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza.
Taarifa hiyo imesema kuwa, jinai kubwa zinazotekelezwa katika Ukanda wa Gaza pamoja na kuzuiwa kuingizwa huko misaada ya dharura ya kibinadamu ni njama iliyopangwa awali kwa ajili ya kuwaua kwa umati Wapalestina wasio na hatia wa ukanda huko. Imesema, kuharibiwa ovyo viwanda vya uzalishaji umeme vya Gaza pamoja na maghala ya chakula na madawa, ni jambo ambalo limefanya kudhaminiwa bidhaa muhimu za Wapalestina kuwa jambo lisilowezekana. Imeendelea kusema kuwa, utawala huo usio na huruma unawachinja kinyama Wapalestina wakiwemo watoto, wanawake na wazee bila ya kuzingatia sheria zozote za kimataifa wala utu.
Taarifa ya Kituo cha Kiislamu cha Uingereza imesema kuwa jambo linalosikitisha zaidi ni kuona jinsi nchi za Kiarabu zilivyokaa kimya mbele ya jinai hizo na kutosheka tu kwa kutoa maneno ya masikitiko yasiyo na maana yoyote. Kituo hicho kimetaka wahusika halisi wa mauaji hayo ya umati wafikishwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Imewataka watu wanaopigania haki na uhuru wa mwanadamu kote ulimwenguni kuwafikishia misaada ya dharura wananchi hao ambao wanakabiliwa na mashambulio ya kinyama na mzingiro wa kidhulma wa Wazayuni.
Taarifa hiyo vilevile imeutaka Umoja wa Ulaya, mabunge ya nchi za Ulaya, vyama vya kisiasa, shakhsia mbalimbali na mashirika ya kutetea haki za binadamu kufanya juhudi za kusimamisha mara moja mashambulio na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia pamoja na kuwafikisha wahusika wakuu wa mauaji hayo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. 346411
captcha