IQNA

Mamufti wa Kiislamu watakiwa kuhudhuria kongamano la kimataifa

10:40 - January 13, 2009
Habari ID: 1730284
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani (Muslim World League) Sheikh Abdullah bin Abdulmushin Turki ametoa wito kwa mamufti, maulamaa na mafuqahaa wa Kiislamu kote duniani kushiriki katika Kongamano la Kimataifa la Fatwa litakalofanyika tarehe 17 Januari mwaka huu katika mji mtakatifu wa Makkah.
Katika taarifa aliyotoa kwenye ukurasa wa intaneti wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani (www.themwl.org), Sheikh Turki amesema, jumuiya hiyo imeandaa mipango maalumu ya kufanikisha kikao hicho cha kimatiafa cha Fatwa. Ameongeza kuwa, mamufti na mafuqahaa katika ulimwengu wa Kiislamu watawasilisha makala katika nyanja kadhaa za fatwa zikiwemo umuhimu wa fatwa na chamgamoto zake katika ulimwengu wa leo. Aidha watajadili suala la athari za kutangaza fatwa katika vyombo vya kisasa vya habari na taathira zake kwa jamii za Kiislamu.
Sheikh Abdullah At-Turki amesisitiza juu ya umuhimu wa kutangazwa fatwa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu na athari za suala hilo katika jamii za Kiislamu. Ameongeza kuwa: "Mafuqahaa na mamufti wanaopaswa kutoa fatwa ni wale tu walio na utaalamu katika nyanja hiyo na walio na uwezo wa kufanya istinbati kuhusu sheria za kidini".
"Kongamano hilo la Kimataifa la Fatwa mjini Makkah litatathmini njia za kuwapiga marufuku mamufti wasio wataalamu kutangaza fatwa kupitia magazeti, intaneti na kanali za televisheni za satalaiti", amesema Sheikh Turki.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani amemaliza taarifa yake kwa kutoa wito kwa vyimbo vya habari kushirikiana zaidi na maulamaa na mamufti katika utangazaji fatwa na kujibu masiala ya kidini na kisheria ya Waislamu. Aidha amevitaka vyombo vya habari kutangaza tu fatwa zinazotolewa na mamufti wataalamu.
Kongamano la Kimatiafa la Fatwa litaanza tarehe 27 Januari mjini Makka kwa hisani na Idara ya Fiqhi ya Jumuiya ya Kiislamu Duniani chini ya usimamizi wa Mfalme Abdullah bin Abdulazizi wa Saudi Arabia. 347004
captcha