IQNA

Jukumu la vituo vya Kiislamu katika kutatua mgogoro wa Gaza

11:43 - January 14, 2009
Habari ID: 1730801
Mgogoro wa hivi sasa wa Gaza umevitwisha jukumu zito na jipya vituo vya Uislamu ambavyo vinaweza kuchukua hatua kadhaa kama vile kupasha habari, kuinua kiwango cha muamko na kuhamasisha watu, kuzishawishi serikali zichukue msimamo wa kuunga mkono na kutuma misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Palestina, na hivyo kuchangia katika kupunguza machungu yanayowakabili wananchi hao kutokana na jinai zinazotekelezwa dhidi yao na utawala haramu wa Israel.
Wanasiasa, wasomi, wanafikra na wanazuoni wa Kiislamu wamekuwa wakizungumza na kutoa mitazamo yao tofauti kuhusiana na hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa na vituo vya Kiislamu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi madhlumu wa Palestina kukabiliana na masaibu yanayowakabili kutokana na unyama wanaofanyiwa na utawala haramu wa Israel.
Kuhusiana na suala hilo, Muhammad Hussein Raiszadeh, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon amesema kuwa vituo vingi vya Kiislamu kikiwemo Chuo Kikuu cha al-Azhar nchini Misri, havijatekeleza majukumu yao kama ilivyotarajiwa na Waislamu kuhusiana na Mgogoro wa Ukanda wa Gaza. Amesema, hii ni katika hali ambayo vituo hivyo vinapasa kutoa mashinikizo dhidi ya serikali zao na kuzifanya zichukue hatua za kusimamisha mauaji ya umati yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi katika ukanda huo.
Huku akisisitiza kwamba ni jukumu la wanazuoni wa Kiislamu kuzishawishi fikra za Waislamu zichukie jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya ndugu zao huko Gaza, Raiszadeh amewataka Mamufti wa Saudi Arabia na Misri pamoja na Mkuu wa Chuo cha al-Azhar, walaani jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi huko Gaza na wakati huohuo kuwashawishi wananchi wa nchi hizo wazishinikize serikali zao ili zichukue msimamo wa kusimamisha unyama unaofanywa na Wazayuni hao dhidi ya Wapalestina.
Katika upande wa pili, Allama Sayyid Muhamad Hussein Fadhlullah, mwanazuoni mashuhuri wa nchini Lebanon licha ya kuwataka wanazuoni na wasomi wa Kiislamu wafanye juhudi za kurejeshwa ardhi za Palestina kwa wamiliki halisi wa ardhi hizo, ametaka kifanyike kikao cha dharura cha wanazuoni wa ulimwengu wa Kiislamu ili kujadili na kutatua mgogoro wa hivi sasa wa Ukanda wa Gaza. 346413
captcha