Kwa mujibu wa gazeti la Al Masri al Youm toleo la Jumatano, Huwaidi amesema kuwa: "Hivi sasa Israel imepenya ndani kabisa katika mfumo wa utawala Misrii kwa kiasi kwamba siasa za nje za Cairo kuhusu masuala ya Palestina na eneo la Mashariki ya Kati zinaratibiwa na makundi ya mashinikizo ya Kizayuni".
Ameongeza kuwa mbali na makundi ya mashinikizo ya Kizayuni, baadhi ya makundi ndani ya Misri hasa ya wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vile vile yanahisi kuwa maslahi yao yatadhaminiwa tu kwa ushirkiano wa Misri na Israel na Marekani. Amesema, wanaounga mkono serikali ya Misri wameitaka ifunge kivuko cha Rafah ili kuishinikiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.
Msomi huyo wa Misri amesema, safari za mara kwa mara za Tzipi Livni Waziri wa Mambo ya Nje wa Utawala wa Kizayuni nchini Misri na kukutana na wakuu wa nchi hiyo ni jambo ambalo limetoa pigo kwa itibari ya Misri katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameto wito kwa viongozi wa Misri wachukue mitazamo huru katika maamuzi ya kieneo na kimataifa. Amesema kuwepo utulivu na amani huko Gaza kutakuwa na maslahi ya kiusalama kwa taifa Misri.
Fahmi Huwaidi amekosoa vikali baadhi ya magazeti ya Misri ambayo yameunga mkono sera za serikali ya Cairo kuhusu Gaza na kufungwa kivuko cha Rafah.
"Ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya magazeti ya Misri yanayofungamana na serikali yanapotosha habari kuhusu matukio ya kieneo. Mfano mzuri ni uamuzi wa magazeti hayo kumkosoa Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na kuandika makala zinazomvunjia heshima", amesema Fahmi Huwaidi . 348285