Tahariri hiyo iliyoandikwa na Raheem al-Faisal, mwandishi wa gazeti hilo chini ya anwani isemayo 'ghadhabu ya Waarabu dhidi ya jinai za Israel iko wapi?' inasema kuwa pamoja na kuwa waandishi, wadadisi na wachambuzi wa mambo ulimwenguni wanasema kuwa maandamano yamekuwa yakifanyika katika nchi za Kiarabu kulaani mauaji ya wakazi wa Ukanda wa Gaza yanayofanywa na utawala wa Israel, lakini mhariri huyo anasema kuwa yeye hajashuhudia maandamano kama hayo, au kwa uchache hayajafanyika kwa kiwango ambacho kinaakisi hali halisi ya mauaji na jinai zinazotekelezwa na utawala huo dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Raheem al-Faisal amesema, jambo ambalo amekuwa akilishuhudia yeye mwenyewe, ni Waarabu kuwasha mishumaa mbele ya majengo kwa ajili ya kuwakumbuka wahanga wa jinai za Wazayuni au kuwatuma wanafunzi mabarabarani kwa ajili ya kusoma mashairi ya kuwashajiisha Wapalestina wenyewe waendelee mbele kupambana na hujuma kali na ya kinyama ya Wazayuni, bila ya kuchukua hatua zozote za maana za kuwasaidia ndugu zao kukabiliana na jinai hizo. Amesema hatua kama hizo kwa yakini haziakisi hata kidogo ghadhabu waliyonayo wananchi wa kawaida wa nchi za Kiarabu kuhusiana na jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia wala ulinzi huko Gaza.
Tahariri ya gazeti la Arab News imesema, maandamano madogomadogo ambayo yamekuwa yakifanyika katika nchi za Kiarabu yamekuwa katika kiwango cha maandamano ambayo kwa kawaida hufanyika katika nchi nyinginezo kwa ajili ya kulalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa kama vile chakula au ongezeko la ushuru na kodi! Imeongeza kuwa, haitoshi kwa watu kutuma ujumbe kupitia vyombo vya habari kwa ajili ya kuwapa moyo Wapalestina wanaoendelea kuuawa kinyama huko Gaza wala misaada ya kibinadamu wanayotumiwa na mashirika mbalimbali ya misaada.
Mhariri huyo anaeendelea kuandika kwamba, iwapo wananchi wa nchi za Kiarabu hawatachukua hatua za dharura kwa ajili ya kuwalazimisha watawala wao waushinikize utawala wa Kizayuni usimamishe mauaji ya kinyama dhidi ya watu wasio na kinga, bila shaka utawala huo utaendelea kuwachinja kinyama Waarabu bila kujali lolote.
Reheem al-Faisal amesema kwamba, mwenendo huu mbovu wa Waarabu wa kuonyesha kimya cha kuaibisha mbele ya jinai zinazotekelzwa kila mara na Wazayuni dhidi ya ndugu zao unapasa kubadilika. Amesema, mamilioni ya Waarabu wanapasa kumwagika mabarabarani usiku na mchana ili kulalamikia jinai hizo za kinyama zinazotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya ndugu zao huko Palestina na kutosimamisha maandamano hayo hadi wakati wa kutekelezwa matakwa yao. Amesisitiza kwamba, migomo inapaswa kufanyika katika nchi zote za Kiarabu ambapo vituo vyote vya kibiashara, yakiwemo maduka, vinapasa kufungwa ili kuwalazimisha watawala wa nchi za Kiarabu kutii matakwa ya wananchi wao badala ya kutii matakwa ya mabwana zao wa nchi za Magharibi.
Ameendelea kusema kuwa, wananchi wa nchi za Kiarabu wanapasa kuzidisha mashinikizo yao dhidi ya serikali zao ili zifunge balozi zote za utawala wa Israel katika nchi za Kiarabu na kusimamisha uhusiano wa aina yoyote ile na utawala huo haramu. Amesema, Waarabu wanaweza kuchukua hatua yenye athari zaidi dhidi ya jinai za utawala haramu wa Israel kwa kususia bidhaa za Marekani na utawala wa Israel pamoja na kukata kabisa mabadilishano ya aina yoyote ile ya kielimu kati ya vyuo vikuu vya nchi za Kiarabu na Marekani.
Mhariri wa gazeti la Arab News amesisitiza kwamba Marekani inapasa kuhisi ghadhabu ya wananchi wa Kiarabu kupitia hatua hizo zenye athari kubwa badala ya kufanya maandamano madogo tu na yasiyokuwa na athari yoyote katika kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Waarabu. 349036