Muhammad ar-Rawi, Mkuu wa Kamati ya Qur'ani na Tafsiri ya Jumuiya ya Utafiti wa Kiislamu ya Chuo Kikuu cha Al-Azhar amesema kuwa, kukubali kamati hiyo usambazwaji wa Qur'ani Tukufu iliyotarjumiwa na Kariman Hamza, mwanamke mtafiti wa Qur'ani wa Misri ni dalili ya wazi inayothibitisha kuwepo usawa na uadilifu kati ya wanawake na wanaume katika kueneza na kuhubiri mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Akizungumza na gazeti la as-Sharqul Ausat, ar-Rawi amesema kuwa, jumuiya hiyo ya utafiti wa Qur'ani ya al-Azhar ndiyo marejeo ya juu zaidi ya kidini katika chuo hicho, marejeo ambayo yanasimamia na kuchunguza kwa makini shughuli zote zinazohusiana na Qur'ani. Amesema, kila neno linalotumika katika kutafsiri na kutarjumu maneno ya Qur'ani huchunguza kwa makini na wakuu wa kamati iliyotajwa ya jumuiya hiyo.
Kuhusiana na suala hilo, Abdudhahir Abu Ghazala amedokeza kuwa tayari juzuu 20 za tafsiri ya bibi huyo mtafiti wa Qura'ni zimeshapata kibali cha kuchapishwa na kusambazwa nchini Misri na kwamba, juzuu zilizobaki bado zinaendelea kuchunguzwa na wahusika. Amesema juzuu zilizopitishwa zinaambatana kabisa na mafundisho pamoja na sheria za Kiislamu na kwamba zinafanana na tafsiri zilizofasiriwa na wataalamu wengine wa kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu.
Abdudhahir Abu Ghazala amekanusha madai ya baadhi ya wafasiri wa Qur'ani nchini Misri kwamba tafsiri hiyo ni mpya na inayozingatia zaidi masuala ya wanawake katika Qur'ani, na kusema kuwa, tafsiri hiyo inazingatia matabaka yote ya Waislamu wakiwemo wanawake, watoto, wanaume, akina mama na vijana na kwa msingi wa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyoandikwa katika kitabu hicho.
Ni muhimu kuashiria hapa kwamba, Taysir al-Tafsir, tafsiri ya kwanza kuandikwa na mwanamke wa Misri kwa jina a Fauqiya Ibrahim as-Sharbini iliruhusiwa kuchapishwa na kusambazwa nchini Misri siku chache zilizopita baada ya kuchunguzwa na jumuiya iliyotajwa kwa muda wa miaka mitatu. Tafsiri hiyo iko katika majalada manne.351252