IQNA

Mahakama ya Rufaa ya Kuwait: Hatibu wa Kishia hana hatia

10:59 - January 21, 2009
Habari ID: 1733938
Mahakama ya Rufaa ya Kuwait imetoa hukumu ikitangaza kwamba haikumpata na hatia yoyote Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Muhammad al Fali, mwanazuoni na hatibu maarufu wa Kishia mwenye asili ya Iran anayeishi nchini humo. Al Fali alikabiliwa na tuhuma ya kuwavunjia heshima masahaba wa Mtume (saw).
Hukumu iliyotolewa na Mkuu wa Mahakama ya Rufaa ya Kuwait Saleh al Murshid imesema: Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammad al Fali hana hatia yoyote na kwamba halazimiki kulipa fidia ya dinari elfu kumi za Kuwait.
Sayyid al Fali alitiwa nguvuni miezi miwili iliyopita katika uwanja wa ndege wa Kuwait kwa tuhuma ya kusambaza CD zenye maelezo yanayowavunjia heshima masahaba wa Mtume na kuchapisha makala inayokebehi matukufu ya Kiislamu katika mtandao wa intaneti. Hatibu huyo wa kishia aliachiwa huru kwa dhamana ya mbunge Saleh Ashur wa Kuwait.
Kadhia hiyo ilizusha mvutano mkubwa kati ya wawakilishi wa kisalafi wenye mitazamo mikali katika bunge la Kuwait na serikali ya nchi hiyo. Wabunge hao walitishia kuisaili serikali iwapo mwanazuoni huyo hatafikishwa mahakamani. Hatimaye Muhammad al Fali alihukumuwa na kufukuzwa Kuwait. Hata hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa imetangaza kuwa Sayyid al Fali hana hatia yoyote.
Kwa upande mwingine Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammad Baqir Muhri ambaye ni miongoni mwa maulamaa wa Kuwait amewashukuru majaji wa Mahakama ya Rufaa ya nchi hiyo kwa kutoa hukumu ya kiadilifu na akawataka wale waliozusha mgogoro huo kumuomba radhi rasmi Waziri Mkuu wa nchi hiyo kupitia vyombo vya habari. Vilevile amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kuwait kumruhusu Muhammad al Fali kuingia tena nchini humo baada ya kutopatikana na hatiya na Mahakama ya Rufaa. 351667
captcha