IQNA

Kanali ya kwanza binafsi ya kidini ya satalaiti yaanzishwa Misri

11:27 - January 25, 2009
Habari ID: 1735263
Kamati ya Masuala ya Kidini katika Bunge la Misri inayoongozwa na Ahmad Omar Hashim imeidhinisha sheria ya kuruhusu kuanzishwa kanali ya kwanza ya televisheni ya satalaiti ya masuala ya kidini isiyokuwa ya serikali.
Kwa mujibu wa gazeti la Al Ahram, Ahmad Omar Hashim amesema kuwa: "Kanali hiyo ya televisheni itaendeshwa na bodi inayojumuisha wataalamu wa masuala ya habari na wafadhili".
Ameongeza kuwa maulamaa wa Kidini na wataalamu wa ulinganiaji wa Kiisalmu wa Misri watakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa kanali hiyo ya televisheni inatekeleza majukumu yake bila kuwepo taasubi na misimamo mikali ya kufurutu mipaka.
"Lengo la kuanzisha kanali hii ya televisheni ya satalaiti ni kuondoa rabsha na ukosefu wa taratibu katika uga wa kutangaza fatuwa, kurekebisha sura ya Uislamu katika nchi za Magharibi, kujibu masuala yenye utata na tuhuma dhidi ya Uislamu kwa mujibu wa misingi na mafunzo ya dini iliyowazi ya Kiislamu, Qur'ani Tukufu na Suna ya Mtume SAW", amesema Ahmad Omar Hashim.
Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kidini katika Bunge la Misri ameongeza kuwa malengo mengine ya kanali hiyo ya satalaiti ni kuchunguza masuala na masaibu ya watu wa Palestina na hasa wakazi wa Ukanda wa Gaza, matatizo ya Waislamu waliowachache katika nchi zisizo za Kiislamu duniani, mazungumzo ya kidini kwa njia za kisasa na katika fremu ya misimamo ya wastani".
Mbunge huyo mwandamizi wa Misri amesema kuwa kanali hiyo ya televisheni itakayorusha matangazo yake kwa satalaiti itajulikana kama Al Wasita na kwamba awali itarusha matangazo yake kwa lugha ya Kirabu kisha baadaye kwa lugha nyinginezo duniani. 353428

captcha