Kwa mujibu wa ukurasa wa habari wa Aljazeera net, Hessam Zaki Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri amesema kuwa: "Misri haikusudii kudhibiti mpaka wa Gaza kwa kutia saini mapatano ya usalama na Israel. Misri pia haitaki kukiuka haki za Wapalestina waishio Gaza.
Ameongeza kuwa, Misri ina majukumu ya kulinda mipaka yake tu na kwa vyovyote vile haitoruhusu vikosi vya kimataifa kuingia katika ardhi yake.
Hessam Zaki amesema, madai ya Israel kuhusu kuwepo mapatano ya amani na Misri ni sehemu ya uzushi wa wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi kwa lengo la kuficha kushindwa jeshi la Israel katika vita vya Gaza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Misri amemaliza kwa kusema kuwa: "Safari ya Amos Gilad Mkuu wa Shirika la Usalama la Wizara ya Vita ya Israel mjini Cairo ilikuwa kwa ajili tu ya kujadili usitishwaji vita daima katika Ukanda wa Gaza, kufunguliwa vivuko vya Gaza na usalama wa mipaka".
Ijumaa iliyopita Amos Gilad alitembelea Cairo akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kijeshi na kisiasa na kukutana na wakuu wa Misri. Baadhi ya duru za habari zimesema, safari ya ujumbe huo wa utawala wa Kizayuni wa Israel ilikuwa kwa ajili ya kutia saini mapatano ya usalama na Misri kuhusu udhibiti wa mipaka ya Gaza. 353393