IQNA

Maonyesho ya ‘mapambano ya watu wa Gaza’ yafunguliwa nchini Libya

11:10 - January 25, 2009
Habari ID: 1735366
Maonyesho ya mabango ya sanaa kwa madhumuni ya kuadhimisha na kusifu mapambano ya kishujaa ya watu wa Ukanda wa Gaza katika kukabiliana na mashambulio ya kinyama ya utawala haramu wa Israel, yamefunguliwa nchini Libya.
Katika maonyesho hayo, wasanii wa Libya wanaonyesho mabango makubwa 60 yaliyo na michoro pamoja na picha za sanaa zenye madhumuni ya kusifu mapambano ya watu wa Gaza pamoja na wapiganaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, dhidi ya mauaji ya umati ya Wazayuni.
Kimya cha watawala wa baadhi ya nchi za Kiislamu na taasisi za kimataifa mbele ya jinai hizo za Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia, ni baadhi ya maudhui zinazojadiliwa na mabango hayo ya wasanii wa Libya.
Adil Jarju’, mmoja wa wasanii wa Libya anayeshiriki katika maonyesho hayo amesema kuwa, mwishoni mwa maonyesho hayo ya wiki moja, mabango hayo yatauzwa kwenye mnada na kisha fedha zitakazopatikana zitatumwa kwa Wapalestina. Amesema, maonyesho hayo ya sanaa ni hatua muhimu katika kuwaunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina na kwamba, uungaji mkono kwa wananchi hao hautimii kwa silaha tu bali pia kupitia maoenyesho kama hayo ya sanaa, uandishi na maneno ya kuwapa moyo katika medani ya vita na kapindi hiki kigumu wanachokabiliwa nacho.
Fauzi al-Suwei, mkuu wa maonyesho hayo amesema kuwa hatua hiyo ya wasanii inaonyesha jinsi jinai za utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza zilivyoathiri na kuwasikitisha wengi katika matabaka yote ya jamii ya Libya. Amesema, sanaa ni njia muhimu mno ya kuwafahamisha watoto wa Libya jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya wenzao huko katika Ukanda wa Gaza na kuamsha miongoni mwao moyo wa mapambano dhidi ya siasa za kujipanua utawala wa Kizayuni katika ardhi za Waarabu. 353239
captcha