Baada ya kutolewa ripoti hiyo ambayo imesisitiza kwamba Waislamu wa madhehebu ya Shia wanabaguliwa na uhuru wao wa kijamii unakiukwa nchini Saudi Arabia, viongozi wa nchi hiyo wameitumia ujumbe Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa wakitangaza kuwa serikali ya Riyadh itafanya jitihada za kuboresha hali ya haki za binadamu na uhuru wa kijamii.
Ujumbe wa viongozi wa Saudia umesema: Kubadilisha baadhi ya ada za zamani za Saudi Arabia kunahitaji hatua na mwenendo makhsusi na kwamba kuoanisha mfumo wa kikabila na kijadi wa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na mazingira ya sasa kunahitajia muda.
Jumamosi iliyopita Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa ripoti katika mji wa Geneva Uswisi ikiituhumu Saudi Arabia kuwa inawabagua Waislamu wa madhehebu ya Shia na kukiuka haki za wanawake na wafanyakazi wa kigeni.
Ripoti hiyo imeashiria kuzuiwa shughuli za kidini za Waislamu wa Kishia, kutiwa nguvuni kwa wingi raia wafuasi wa madhehebu hiyo kwa sababu ya kutekeleza ibada na shughuli zao za kidini na ukiukwaji wa haki za kijamii za wanawake katika jamii ya Saudi Arabia.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema: Saudi Arabia ndiyo nchi mbaya zaidi duniani katika suala la ukiukaji wa uhuru wa kijamii na kiraia.
Kikao cha Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa yenye wanachama 192 kimepangwa kufanyika tena tarehe 26 mwezi huu wa Februari mjini Geneva kujadili hali ya haki za binadamu katika nchi mbalimabli duniani. 353875