Hayo yamesema na Waziri wa Habari wa Yemen Hassan al-Lawzi katika kikao cha Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu huko Rabat Morocco.
Ameongeza kuwa: “Umma wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto na matatizo mengi kutokana na maisha ya dunia ya leo na vyombo vya habari vya Kiislamu vinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuleta mshikamano na umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu”.
Ameongeza kuwa: “Kuzuia kuenea fikra potofu na zilizo kinyume cha itikadi za Kiislamu, kuhimiza umoja wa Kiislamu, uhuru, demokrasia na kuvunja njama za maadui za kuzusha mifarakano ya kikaumu, kimadhehebu na kikabila ni kati ya majukumu muhimu ya vyombo vya habari vya Ulimwengu wa Kiislamu”.
Hassan al-Lawzi amekumbusha kuwa: “Vyombo vya habari vya Yemen vinaendesha shughuli zao kwa msingi wa thamani za Kiislamu na vinajaribu kuimarisha umoja wa kitaifa na Kiislamu na kwamba vina mipango mingi katika uga wa kustawisha mshikamano wa Kiislamu, kulinda utambulisho na utamaduni wa Kiislamu pamoja na kushirikiana kiuchumi na kusaidiana kihabari jamii za Kiislamu”.
Amesema kuwa, hivi sasa Umma wa Kiislamu unakabiliwa na hujuma kali ya vyombo vya habari vya Magharibi na Waislamu wanapaswa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi katika uwanja wa habari na mawasiliano ili wafanikiwe kukabiliana na adui. ‘Ili kustawisha ulimwengu wa Kiislamu kijamii na kiuchumi kuna haja ya kukabiliana na umasikini, njaa na kujitahidi kuimarisha thamani za usawa, udugu na haki za binaadamu’, amesema waziri huyo wa Yemen. 355655