Kwa mujibu wa gazeti la nchi hiyo la ad-Dar, Swaleh Ashur, mwakilishi wa Kishia katika Bunge la Kuwait amesema kuwa Mashia wa nchi hiyo wanabaguliwa na kukabiliwa na vikwazo vingi mno kutoka kwa idara za serikali katika juhudi zao za kujenga misikiti, vituo vya kidini pamoja na kutekeleza minasaba mbalimbali ya madhehebu yao. Ameitaka Wizara ya Wakfu ya Kuwait pamoja na vyombo vingine vya utendaji vya serikali kubadili sheria zao kuhusiana na maombi yanayotolewa na Mashia kuhusiana na haja ya kujenga misiki pamoja na vituo vyao vingine vya kimadhehebu na kuamiliana nao kwa uadilifu kama wanavyofanyiwa wafuasi wa madhehebu ya Kisuni nchini humo.
Huku akiashiria kwamba viongozi tofauti wa serikali wanaamiliana kwa njia tofauti na maombi hayo, Swaleh Ashur amesisitiza kwamba serikali inapasa kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kukomesha kabisa ubaguzi unaotekelezwa na viongozi wengi wa serikali dhidi ya Mashia, ili kuwaruhusu watekeleze kwa uhuru kamili majukumu na nyadhifa zao za kidini bila kunyanyaswa na mtu yoyote.
Baraza la Mji wa Kuwait hivi karibuni lilifutilia mbali kibali kilichokuwa kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Ahlul Beit (as) mjini Kuwait, jambo ambalo linapingana moja kwa moja na mada ya 12 ya katiba ya nchi hiyo. 357336