IQNA

Amr Musa atetea kimya chake katika kikao cha Davos

9:05 - February 03, 2009
Habari ID: 1739330
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Amr Musa ambaye yuko chini ya mashinikizo ya umma katika Ulimwengu wa Kiarabu kutokana na hatua yake ya kubakia katika kikao cha Davos Uswisi hata baada ya Waziri Mkuu wa Uturuki Rajab Tayyib Erdogan kuondoka, ametetea uamuzi wake kwa kudai kuwa: “Erdogan aliondoka katika kikao cha Davos kwa ajili ya usimamizi mbovu wa mdahalo na si kwa ajili ya masuala ya kisiasa na kulalamikia matamshi ya Rais wa utawala haramu wa Israel Shimon Peres”.
Katika mahojiano na gazeti la al-Sharq al Ausat, Musa ameongeza kuwa: “Iwapo ningefahamu kuwa Erdogan aliondoka katika kikao hicho kwa ajili ya kulalamikia matamshi ya Peres na hatua ya hadhirina kumpigia makofi kiongozi wa Israel, mimi pia ningefanya hivyo”.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ametetea hatua yake ya kuendelea kubakia katika kikao cha Davos na kusema: “Kushiriki Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika vikao vyote vya kimatiafa ni jambo la dharura na fursa kwa ajili ya kujibu madai ya uongo ya vyombo vya habari vya Israel”.
“Katika kikao cha Davos nilibainisha wazi msimamo wa nchi za Kiarabu kuhusu kadhia ya Gaza na kuwafahamisha walimwengu kuhusu jinai za kinyama za utawala a Kizayuni katika Ukanda wa Gaza!” amesema Amr Musa.
Katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema kuwa amekosolewa kwa kukaa pembeni ya Shimon Peres Rais wa Utawala wa Kizayuni katika kikao cha Davos katika hali ambayo kushiriki katika kikao hicho lilikuwa jambo la dharura. “Lazima tujibu madai ya Israel kuhusu hujuma yake huko Gaza pamoja kutetea maslahi ya umma wa Kiarabu”, amesema Musa.
Itakumbukwa kuwa Alhamisi iliyopita, Waziri Mkuu wa Uturuki Rajab Tayyib Erdogan aliondoka katika kikao cha kujadili kadhia ya Gaza huko Davos Uswisi kulalamikia matamshi ya uongo ya Shimon Peres Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni. Erdogan alimwambia bayana Peres kuwa: “Wewe wajua tu kuuwa wanawake na watoto wasio na hatia”, na katika hatua ya kulalamikia mwendeshaji wa kikao aliyekataa kumpa wakati wa kutosha kujibu madai ya Peres, Erdogan aliondoka katika ukumbi wa mdahalo. Hata hivyo Amr Musa hakuondoka katika kikao hicho.
Katika siku za hivi karibuni Amr Musa amekosolewa na wanaharakati wengi wa Kiarabu na Kiislamu kwa kuendelea kubakia katika kikao hicho na kuketi pembeni mwa Rais wa Utawala wa Kizayuni. Wengi wanasema angeondoka pamoja na Erdogan katika kikao hicho. 358088
captcha