John Holmes, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia misaada ya kibinadamu amesema kuwa, jinai za hivi karibuni za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza ni ishara ya wazi kwamba jamii ya kimataifa imeshindwa kutekeleza vilivyo majukumu yake na kwamba inatupasa tukiri kuwa hakuna maendeleo yoyote ambayo yamepatikana kwa ajili ya kutatua kisiasa suala la Palestina.
Amesema kutokana na ukweli huo, hali ya ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel inaendelea kuwa mbaya zaidi.
Akizungumza mjini Geneva Uswisi katika mkutano na waandishi habari akiwa na Karen Abu Zaid, Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Palestina UNRWA, Bwana Holmes amesema kuwa, utawala wa Israel na Misri hadi sasa zimekataa kuruhusu kuingizwa katika Ukanda wa Gaza misaada ya dharura ya kibinadamu inayotolewa na nchi, mashirika pamoja na jumuiya mbalimbali za kimataifa. Amesema, kusimamishwa mara moja kwa mshambulio ya Israel na kufunguliwa kwa vivuko vyote vya Ukanda wa Gaza na kutoingiliwa kisiasa shughuli za misaada ya kibinadamu inayopelekwa katika ukanda huo, ni miongoni mwa masharti muhimu ya kuboreshwa hali ya kibinadamu pamoja na huduma za dharura kwa wakazi wa Ukanda huo.
John Holmes amesisitiza kwamba, vivuko vya Ukanda wa Gaza havipasi kufunguliwa kwa muda tu bali vinapasa kubaki hivyo daima kwa ajili ya kuruhusu uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa maslahi ya wakazi wa ukanda huo.
Mwishoni, ameashiria hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuharibu na kulipua ofisi za mashirika ya kimataifa, zikiwemo za Umoja wa Mataifa za UNRWA katika hujuma yake ya kinyama ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, kamati za uchunguzi za umoja huo zimeanza kufanya uchunguzi mkubwa wa jinai za utawala huo huko Gaza, ambapo matokeo yake yanatazamiwa kutangazwa hadharani baadaye. 358724