Hayo yamesemwa na Sayyid Ihsan Fadhlizadeh, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Croatia na kuongeza kuwa, baada ya mapinduzi hayo, Iran ilikabiliwa na mashinikizo pamoja na vikwazo vingi vya kimataifa vya kisiasa, kiuchumi, hujuma ya utamaduni na vita vya kulazimishwa vya Iraq, jambo lililoifanya itafute njia ya kujitawala na kuwategemea wataalamu wake wa ndani katika njia ya kufikia maendeleo na ustawi uliohitajika nchini.
Fadhlizadeh amesema, jambo hilo katika kipindi cha miaka 30 tu limeipelekea Iran kuwa nguvu kubwa ya kieneo na kimataifa. Amesema, sera hizo za kishujaa za Iran zimehuisha moyo wa kujitegemea, kujitawala na kupambana na dhulma katika nchi nyingi za ulimwengu wa Kiislamu na zisizo za Kiislamu na kwamba, limeifanya Iran ya Kiislamu itazamwe na kuzingatiwa na wengi duniani kuwa nchi yenye nguvu kubwa inayoweza kusimama kidete mbele ya nchi za kibeberu za Magharibi. Amesema, athari za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hii leo zinaonekana katika harakati nyingi za kupigania uhuru na kujitawala katika nchi za Kiislamu za Asia na Afrika.
Huku akibainisha matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kujikwamua kutoka kwenye minyororo ya madola ya kibeberu ya Magharibi, Fadhlizadeh amesema kuwa katika zama ambazo madola hayo na hasa Marekani yamekuwa yakizinyongesha nchi dhaifu duniani na kuzitaka kufuata kibubusa maamrisho yao, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalileta mtazamo na mfumo mpya wa kupigania uhuru ambao umekuwa ukitegemea matakwa ya wananchi wake katika utekelezaji wa kila jambo.
Mtaalamu huyo wa masuala ya kiutamaduni amesisitiza kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyoongozwa na hayati Imam Khomeini (MA) yaliamsha na kuhuisha moyo wa umaanawi na thamani za kidini ulimwenguni ambapo Waislamu walianza tena kujifaharisha na kuwa kwao Waislamu na sio kama walivyokuwa wakidhalilishwa na nchi za Magharibi kabla ya hapo. 358220