Hayo yamesemwa na Muna Nur az-Zilzila, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Bunge la Iraq ambaye ameongeza kuwa fikra mbili za kumbana mwanamke katika kuta za nyumba na nyingine ya kumpa uhuru usio na mipaka, zinaweza kuoanishwa na kutokea fikra ya tatu ambayo ni ya wastani na inayoambatana na mafundisho ya dini na vilevile sheria zilizobuniwa na mwanadamu kuhusiana na mwanamke. Amebainisha hali ya mwanamke wa Iraq iliyokuwepo nchini humo kabla na baada ya kung'olewa madarakani dikteta Saddam Hussein na kusema kuwa, katika kipindi cha utawala wa dikteta huyo, mwanamke alikuwa hapewi nafasi yoyote ya kujiendeleza bali alikuwa ni mfuasi wa mumewe tu, lakini baada ya kuondolewa madarakani dikteta huyo, hali imebadilika sana na kumpa mwanamke uhuru wa kujiendeleza katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kielimu, kiuchumi, kisiasa na kisanaa.
Bi az-Zilzila anaamini kwamba, mwanamke Muislamu wa Iraq katika miongo mitatu iliyopita hakuwa na uwezo wa kujishughulisha na harakati za Kiislamu kutokana na mazingira magumu na mbano mkubwa aliokuwa akiwekewa na utawala wa Saddam Hussein na kwamba alilazimika kuwa mwanachama wa kundi la fikra potofu la ubaathi wa kikomunisti ulioenezwa nchini na watawala wa Chama cha Baath.
Bi az- Zilzila ambaye anashiriki katika kikao cha kwanza cha kimataifa cha 'uchunguzi wa mlingano wa sheria za familia katika nchi za Kiislamu' kinachoendelea mjini Tehran, amesema kuwa, hii leo wanawake wa Iraq wamepata fursa ya kujishughulisha na masuala mbalimbali, zikiwemo harakati za Kiislamu, kwa ajili ya kuimarisha jamii ya wanawake wa nchi hiyo. Amesisitiza kwamba, maendeleo ambayo wanawake wa Kiislamu wa Iraq wameyafikia katika kipindi hiki kifupi yamewashangaza wengi ambao walikuwa wakidai kwamba mwanamke wa Kiislamu hawezi kufikia maendeleo kama hayo isipokuwa anapoamua kuachana na misingi pamoja na sheria za dini yake tukufu.
Az-Zilzila amesema, kinyume na maadai ya maadui wa Uislamu, mafundisho ya Kiislamu ni jambo muhimu linalompa mwanamke moyo wa kujiamini na kujiendeleza katika nyanja mbalimbali katika jamii anayoishi. Amesema, ukweli huo unaonekana wazi nchini Iran ambapo mwanamke ana uhuru mkubwa wa kujishughulisha na suala lolote lile katika jamii na katika kivuli cha sheria za Kiislamu kwa lengo la kuinufaisha jamii na nchi yake. 360893