Abdullah Abdul Muhsin at-Turki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ulimwengu wa Kiislamu amesema katika kikao cha kimataifa cha ‘Vyombo vya Habari vya Zama Hizi, Uhuru wa Kusema na Dharau dhidi ya Dini’ kinachofanyika huko Sanaa, mji mkuu wa Yemen kwamba, Uislamu umekuwa fikra yenye nguvu kubwa zaidi inayojadiliwa na wengi katika nchi za Magharibi.
At-Turki amesema kuwa, mjadala kuhusu Uislamu na maisha ya Kiislamu ni mjadala mkubwa zaidi wa kifikra, kipropaganda na kisiasa unaoendelea sasa katika nchi za Magharibi na kwamba athari za mjadala huo pia zinahisika katika ulimwengu wa Kiislamu.
Sheikh at-Turki ameendelea kusema kuwa, Uislamu ni chanzo muhimu cha maadili na kuongeza kwamba, kupotoshwa mafundisho halisi ya kidini kumepelekea baadhi ya watu kudai kuwa dini ndicho nchonzo cha kuenea machafuko na ghasia katika jamii ya mwanadamu na udugu na urafiki miongoni mwao.
Viongozi wa Kiislamu na kiserikali akiwemo Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Yemen ni miongozi mwa watu waliohutubia kikao hicho. Vita vya Msalaba na athari zake katika kupotosha Uislamu, athari mbaya za vyombo vya habari kwa thamani za kimaadili, uhuru wa kusema na sheria zake katika mtazamo wa dini, maana ya uhuru wa kusema katika Uislamu katika mtazamo wa sunna za Mtume (saw) na katika mtazamo wa utamaduni wa Magharibi ni miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika kikao hicho.
Kikao hicho kimeandaliwa na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Yemen kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ulimwengu wa Kiislamu. Zaidi ya wasomi na wanafikra wa Kiislamu na wasiokuwa Waislamu 200 wanashiriki katika kikao hicho.
Kama tulivyotangulia kuashiria hapo juu, kikao hicho kinachunguza nafasi ya vyombo vya habari katika zama hizi katika kudharauliwa na kutusiwa itikadi na thamani za kidini. 361371