IQNA

Kikao cha sita cha Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu chaanza nchini Qatar

12:50 - February 15, 2009
Habari ID: 1744185
Kikao cha sita cha Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu kimeanza katika hoteli ya Four Seasons mjini Doha Qatar.
Kwa mujibu wa gazeti la Peninsula, wawakilishi na viongozi wa mashirika na taasisi za kisiasa, kibiashara, vyombo vya habari, vyuo vikuu na jumuiya za kiraia wanashiriki katika kikao hicho cha siku tatu ambacho kitajadili masuala mbalimbali yanayohusiana na changamoto pamoja na matatizo mahimu yaliyopo kati ya Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu.
Shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na warsha za mafunzo zitaendelea pambizoni mwa kikao hicho.
Kwa mara ya kwanza kabisa, kitengo maalumu cha vijana walio na umri wa chini ya miaka 30 ambao wanaunda asilimia 60 ya jamii ya nchi za Kiislamu kimeanzishwa katika kikao hicho. Maoni ya vijana hao ambao ni viongozi wa baadaye wa Ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na masuala mbalimbali yatachunguzwa na kupewa umuhimu.
Baadhi ya masuala yatakayojadiliwa katika kikao hicho ni uchunguzi wa masuala ya kiutamaduni ya ulimwengu wa Kiislamu, mivutano ya Waarabu na utawala haramu wa Israel, mgogoro wa kiuchumi duniani, suala la kudhaminiwa nishati katika karne ya 21, jamii iliyoelimika, na athari za kuwepo Rais Obama katika White House kwa Ulimwengu wa Kiislamu . 363723
captcha